#SheriaYaLeo (85/366); Jenga uwezo wa kupokea usiyokubaliana nayo.

Ni kawaida kwetu binadamu tukishajenga mazoea fulani ndiyo huwa tunaendelea nayo.
Tunaona hiyo ndiyo namna sahihi ya kufanya kitu husika.

Pale tunapokutana na namna ya tofauti na tulivyozoea, huwa tunaikosoa na kuipinga kwamba siyo sahihi.
Tunatetea namna yetu kwa kuona ndiyo sahihi zaidi.

Hili huwa ni kikwazo kikubwa kwenye ukuaji zaidi na kufikia ubobezi wa hali ya juu.
Ili kubobea na kubaki kwenye ubobezi, lazima uweze kupokea hata vitu usivyokubaliana navyo bila ya kuvipinga au kuvishambulia.
Unapaswa kuvichunguza kwa kina na kujifunza kwa undani ili uweze kutoka na namna ya kwenda kuboresha zaidi kile unachofanya.

Hata kama ni kitu kinachopingana kabisa na vile unavyoamini au ulivyozoea wewe, usikidharau na kukikataa.
Badala yake kuwa tayari kukipokea, kujifunza kwa undani na kuondoka na mambo unayoweza kufanyia kazi ili kuwa bora zaidi.

Epuka sana kuwa na itikadi fulani au mtazamo mgando kwenye kile unachofanya.
Iruhusu akili yako kupokea mawazo mbadala, kujifunza na kisha kuwa bora zaidi.

Sheria ya leo; Jijengee tabia ya kuepuka kuhukumu kila kitu unachokutana nacho. Pokea na jifunze mawazo mbadala yanayokinzana na ulivyozoea na unavyoamini. Jifunze na ona unavyoweza kutumia hayo kuboresha zaidi kile unachofanya.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji