2582; Nafasi ya kujua ujinga wako.

Bradley Sugars kwenye kitabu cha Billionaire in Training anashirikisha nukuu inayosema; watu wengi huwa wanafikiri mabosi wao ni wajinga, mpaka pale wanapokuja kuwa mabosi wao wenyewe.

Ni rahisi sana unapoona mtu mwenye nafasi fulani anakosea kwa maamuzi anayokuwa anafanya.
Lakini unapokuja kuwa kwenye nafasi kama yake, ndiyo unaona ni jinsi gani unalazimika kufanya maamuzi ambayo wengine wanaona hayafai.

Huo ndiyo ugumu wa kuwa kiongozi au msimamizi.
Kwa namna yoyote ile hakuna maamuzi utakayoweza kufanya na yakamridhisha kila mtu.
Lazima kuna watu ambao hawataridhika na maamuzi yako na kukuona wewe ni mjinga na usiyefaa.

Ukitaka kuwa kiongozi wa hovyo kabisa na ambaye anadharaulika na kila mtu, jaribu kutaka kumridhisha kila mtu.
Unapofanya kitu fulani na baadhi ya watu wakalalamika, haraka kimbilia kufanya kitu cha tofauti ili kuwaridhisha watu hao.
Utaishia kutokumridhisha yeyote na hata wewe mwenyewe hutaridhika.

Utajikuta ukihangaika na mambo mengi lakini hakuna hatua yoyote kubwa unayokuwa umepiga.
Hiyo ni kwa sababu kila mara kuna moto unazima, kila wakati kuna watu unataka kuwaridhisha, ambao pia baada ya muda hata hawajali.

Kuepuka hilo, kiongozi unapaswa kuwa na maono. Maono ndiyo yakuongoze kwenye kila unachofanya.
Unapofanya kwa maono, kuna wengi ambao hawataridhika, ambao watakuona wewe ni mjinga na usiyefaa.

Lakini matokeo mazuri yatakapoonekana kwa wewe kuyasimamia maono yako, kila mtu atayafurahia na wote watakuheshimu.

Hatua ya kuchukua;
Usiwe mwepesi wa kuhukumu wengine kwa yale wanayofanya kama hujui kwa undani nini kimewasukuma wafanye.
Pia ongozwa maono na ndoto zako kubwa kwenye kila maamuzi unayofanya. Hata kama hayawaridhishi wengi, kama yanakufikisha kwenye maono uliyonayo, hayo ndiyo sahihi.

Tafakari;
Kutaka kumridhisha kila mtu ni kuishia kutokumridhisha yeyote. Angalau jiridhishe wewe mwenyewe kwa kuyasimamia maono yako makubwa.

Kocha.