#SheriaYaLeo (87/366); Nguvu ya kuzama kwenye ufanyaji.

Ugumu mkubwa uliopo kwenye safari ya ubobezi ni muda mrefu unaohitajika kwenye kufanya kile ulichochagua kufanya.

Huku pia ukiwa unashawishiwa na tamaa mbalimbali za vitu vinavyoweza kuwa na manufaa ya muda mfupi ila siyo ya muda mrefu.

Unalazimika ujitoe kweli kweli na utoe kafara nyingi ili uendelee kubaki kwenye kile ulichochagua.
Utakutana na uchovu mkali na wakati mwingine kutaka kukata tamaa.

Kuvuka hayo, unapaswa kutumia nguvu ya kuzama kwenye ufanyaji. Hii inaitwa hali ya flow, ambapo umakini wako wote unakuwa kwenye kile unachofanya na unasahau kabisa mengine.
Unapata nguvu ya kufanya kitu kwa muda mtefu bila ya kuchoka au kujali ni muda kiasi gani umefanya.

Kwenye hali hiyo ya flow, akili yako inakuwa imezama kweli kwenye kile unachofanya, unakuwa na utulivu wa hali ya juu kabisa na unafurahia kweli kile unachofanya kiasi kwamba hutaki kuacha kufanya.

Utakuwa na ufanisi na uzalishaji mkubwa kwenye hali hiyo ya flow kuliko unavyokuwa kwenye hali nyingine.
Utapata msukumo wa kuendelea kutengeneza hali za aina hiyo mara kwa mara maana unayaona manufaa yake.

Pamoja na kwamba itakulazimu uachane na mambo mengine, lakini matokeo unayoyapata yanafidia kile unachokuwa umekikosa.

Sheria ya leo; Ingia kwenye hali ya flow leo. Tenga muda wa kufanya kitu na weka akili yako yote kwenye kitu hicho. Ondokana na kila aina ya usumbufu unaotaka kukutoa kwenye kile unachofanya. Jisahau kabisa wewe na zama kwenye kile unachofanya.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji