#SheriaYaLeo (90/366); Ona Zaidi Ya Kinachoonekana.
Watu wa kawaida ambao hawajafikia ubobezi, huwa wanaona yale tu yanayoonekana.
Hiyo ni kwa sababu wanakuwa hawajaweka umakini mkubwa kwenye kitu na kukielewa kwa undani.
Lakini wale waliofikia ubobezi wa hali ya juu kwenye kile wanachofanya, huwa wanaona zaidi ya kinachoonekana.
Kwa sababu wanakuwa wameweka umakini mkubwa na kuzama ndani kabisa, wanakuwa wamejijengea machale makubwa.
Machale hayo yanawawezesha kutumia hisia na roho kuelewa vitu, badala tu ya akili kama ilivyo kwa wengine.
Wanaweza kuhisi kitu hakipo sawa na kweli kikawa hakipo sawa, wakati wengine hawana uwezo wa aina hiyo.
Kufikia ngazi hii ya kuweza kuona zaidi ya yanayoonekana, lazima uzame ndani kwenye kile unachofanya na ukijue kwa kina.
Unapaswa pia kuyaamini machale yako, pale unapohisi kitu fulani, pale nafsi yako inapokuonyesha kitu hata kama kifikra hakionekani usiipuuze, amini na fanyia kazi yale yanayokujia.
Utashangaa jinsi ambavyo utaweza kuona na kufanya mambo ambayo watu wengine hawayawezi.
Na hilo litazidi kukuweka kwenye ubobezi wa hali ya juu, maana unafanya vitu kwa namna ambayo wengine hawawezi kufanya.
Sheria ya leo; Kadiri unavyokaa kwenye njia ya ubobezi, ndivyo unavyoelewa kwa kina na ndivyo nguvu ya kuona zaidi ya yanayoonekana inavyozidi kuwa imara.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji