Rafiki yangu mpendwa,
Kuna vitu viwili ambavyo vinagusa maisha ya kila binadamu hapa duniani.
Vitu hivyo ni WAJIBU na UDHIBITI.
Wajibu ni kile tunachopaswa kufanya. Wale wanaokubali na kufanya wanachopaswa kufanya huwa wanapata matokeo mazuri. Lakini wapo ambao hawakubali wajibu wao, wakitafuta njia za kukwepa na kujificha, hao hawakuna makubwa wanayoweza kufanya.
Na udhibiti ni nguvu ya maamuzi tuliyonayo kwenye kitu. Walio tayari kufanya maamuzi kwa namna wanavyotaka ndiyo wanaozalisha matokeo makubwa. Wanaokwepa kufanya maamuzi kwa sababu hawataki lawama hakuna makubwa wanayofanya.
Sasa kwa kuchanganya vitu hivyo viwili kwa pamoja, tunapata makundi manne ya watu.

Kundi la kwanza ni la waathirika (victims).
Hawa ni ambao hawana udhibiti na hawataki wajibu.
Hawa ni watu ambao hakuna chochote kikubwa wanachofanya na hawana udhibiti wowote.
Hawa ni watu wa bora liende tu, wakiwa hawana ndoto zozote kubwa wanazopigania.
Kundi hili ndipo walipo wengi, ambao hujikuta wakizurura hapa duniani mpaka maisha yao yanaisha wakiwa hawajayaishi.
Kundi la pili ni la walalamikaji (whiners).
Hawa ni ambao wana udhibiti mkubwa ila hawataki wajibu wowote.
Wanakwepa majukumu lakini ni wazuri sana kwenye kulalamikia wengine.
Hujiona ni muhimu na wanaostahili kuliko wengine.
Hupaza sauti sana, lakini hakuna wanachofanya.
Kundi hili limejaa wanasiasa na watu wengine ambao ni waongeaji kuliko wafanyaji.
Kundi la tatu mashahidi (martyr).
Hawa wana wajibu mkubwa ila udhibiti mdogo.
Ni watu wanaojali kupitiliza kuhusu kile wanachofanya, ila hawana mamlaka makubwa kwenye kitu hicho.
Hawa kuwa tayari kufia kitu hicho, kwa sababu wanakikubali na kukiamini sana.
Kundi hili lina watu wanaofanya kazi za wito ila hawana mamlaka.
Kundi la nne ni viongozi (leaders)
Hawa wana wajibu mkubwa na udhibiti mkubwa pia.
Wana mamlaka na wanachukua majukumu.
Wanatumia mamlaka yao kuchukua hatua zenye manufaa kwa wengine.
Hata pale mambo yanapokwenda vibaya, hawalalamiki, bali wanawajibika.
Hili ndiyo kundi ambalo viongozi bora wapo. Ni kundi lenye watu wachache, lakini wanaoleta mapinduzi makubwa kwenye kile wanachofanya.
Rafiki, kwenye hayo makundi manne ni kundi lipi ulipo kwa sasa?
Jipime wewe mwenyewe ni udhibiti kiasi gani ulionao na hatua zipi unazochukua?
Siyo lazima tu iwe kwenye kazi au biashara unayofanya, bali hata kwenye maisha yako binafsi.
Je pale mambo yanapokwenda tofauti na ulivyotegemea huwa unafanya nini?
Unakubali huo ni wajibu wako na kuchukua hatua kubadili hilo?
Au unalalamika na kulaumu wengine kwa kinachokuwa kimetokea?
Rafiki, kundi sahihi kwako kuwa ni kwenye kundi la viongozi.
Hilo ndiyo kundi litakalokuwezesha kufanya makubwa kwenye maisha yako na kufika kule unakotaka.
Na huhitaji kuzaliwa kiongozi ndiyo uwe kwenye kundi hilo.
Bali unahitaji kushika hatamu ya vitu viwili, WAJIBU na UDHIBITI.
Chagua kuwajibika na kutekeleza majukumu yako.
Na pia chagua kuwa na udhibiti kwenye kila eneo la maisha yako.
Hata kama kwa sasa huna kabisa vitu hivyo viwili unaweza kuanza kuvijenga sasa kidogo kidogo.
Kadiri unavyojijengea ndivyo inavyokuwa tabia na kukuwezesha kufanya makubwa.
Tayari ndani yako una nguvu kubwa ya kuweza kufanya makubwa unayotaka.
Inaweza kuwa imelala kwa sababu kwa muda mrefu hujaitumia.
Ni wakati sasa wa kuamsha nguvu hiyo ili uweze kufanya makubwa.
Jipatie na usome kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA ili uweze kuifikia nguvu yako ya ndani na uitumie kufanya makubwa.
Wasiliana sasa na namba 0752 977 170 kujipatia nakala yako.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Muuza Matumaini, Kocha Dr Makirita Amani.