2588; Hisia kwanza.

Sisi binadamu ni viumbe wa kihisia.
Pamoja na uwezo mkubwa wa ubongo wetu kufikiri na kufanya maamuzi, bado kwa sehemu kubwa tunaendeshwa na hisia kuliko fikra.

Badala ya kuamua kwa fikra kisha kuweka hisia katika maamuzi yetu.
Huwa tunaamua kwa hisia kisha kuhalalisha kwa fikra.
Hivyo haijalishi kama maamuzi ni sahihi au la, tukishaamua tunatafuta fikra za kuyahalalisha, na huwa hatuzikosi.

Elewa na utumie hili kwa pande mbili.

Upande wa kwanza ni wewe mwenyewe. Katika kufanya maamuzi, jilazimishe sana kuyafanya kwa fikra kisha ndiyo uweke hisia.
Jijengee utaratibu na vigezo utakavyolazimika kuvifuata wakati wa kufanya maamuzi.
Mara zote usiende nje ya vigezo hivyo, hata kama utashawishika vipi.
Hata kama utaona unakosa fursa nzuri, ikose tu.
Sheria na vigezo ulivyojiwekea vitakukosesha baadhi ya fursa nzuri, lakini vitakuokoa usianguke kwenye fursa mbaya.

Upande wa pili ni watu wengine. Katika kuwashawishi watu, tumia hisia badala ya fikra/mantiki. Waambie watu kile wanachotaka kusikia, kile kinachowafanya wajisikie vizuri.
Kadiri unavyowateka watu hisia zao, ndivyo wanavyosukumwa kukubaliana na wewe kwenye kile unachowashawishi.
Haijalishi kuna mantiki nzuri kiasi gani, kama inakwenda kinyume na hisia ambazo mtu anataka au anazo, haitaweza kumshawishi.
Na unachotaka ni ushawishi kwanza, kisha mantiki inaweza kufuata.

Hatua ya kuchukua;
Jiwekee sheria na vigezo utakavyotumia kwenye kila maamuzi unayofanya na kuwa na mtu anayekuwajibisha kuhakikisha unavitumia kwenye kufanya maamuzi.
Unapotaka kuwashawishi wengine, jua kwanza nini wanataka kusikia au wanapendelea, kisha tumia hayo katika kuwashawishi.

Tafakari;
Hisia zina nguvu kuliko mantiki, jijengee hisia sahihi ambazo zitachochea kufika kule unakotaka. Kila mara angalia namna unaweza kutumia hisia kupata unachotaka, kwako na kwa wengine pia.

Kocha.