Rafiki yangu mpendwa,

Mtaji wa fedha ni moja ya rasilimali muhimu ambayo inahitajika sana kwenye kuanza na kukuza biashara.

Mtaji huwa ni rasilimali ambayo kila wakati ina uhaba.
Wakati wa kuanza biashara unaweza usiwe nayo au isitoshe.
Na hata ukishaanza, kuikuza zaidi biashara pia itahitaji mtaji zaidi.

Watu wamekuwa wakitumia njia mbalimbali za kupata mtaji wa biashara, baadhi ni nzuri na baadhi siyo nzuri.

Kwenye makala hii ya ushauri tutaona kama njia aliyouliza mwenzuri ni nzuri au la.

Kabla hatujaingia kwa undani kuiangalia, tusome alichoandika menzetu.

“Kuuza kiwanja na pesa kuifanyia biashara ni jambo zuri?” – A. Z. Arzola

Kama alivyoandika mwenzetu hapo, kuna wengine wengi wanajikuta kwenye njia panda hiyo, huna mtaji wa biashara ila kuna mali unayo kama kiwanja au nyumba.

Ukiangalia mali hiyo ni pesa tu zimelala, au kama wengine wanavyoita zimezikwa.
Unashawishika ukiuza na kuzungusha hiyo fedha utaweza kutengeneza faida kubwa.

Swali ni je hayo ni maamuzi sahihi kufanya?
Na hapo jibu ni ndiyo na hapana.

Jibu ni hapana kama unakwenda kuanza biashara mpya kabisa au biashara ambayo huwa udhibiti nayo.

Iko hivi rafiki, biashara zote kwenye karatasi (wakati wa kupanga) huwa zinaingiza faida.
Lakini kwenye uhalisia biashara nyingi zinaingiza hasara.

Kuanza biashara mpya hakuna tofauti sana na kucheza kamari.
Kuna mengi hujui ambayo utakwenda kujifunza kwa kuingia kwenye biashara.

Sasa hupaswi kucheza kamari hiyo kwa fedha ambayo haupo tayari kuipoteza.

Ndiyo maana benki haikukopeshi fedha ya kwenda kuanzisha biashara.
Inakutaka kwanza uwe umeshaanza biashara ili wakikupa fedha uende ukaitumie kwa uhakika, kwa sababu unajua nini kinafanya kazi na nini hakifanyi kazi.

Hivyo usiuze kiwanja chako ili kupata mtaji wa kwenda kuanza biashara, utapoteza kiwanja na biashara, halafu utakuwa umerudi sifuri.

Kwa kifupi naweza kusema usianze biashara na mtaji ambao huwezi kupoteza. Na unapoingia kwenye biashara, pambana kila namna usipoteze mtaji ulioingia nao.

Jibu pia ni hapana kama biashara unayokwenda kufanya huna udhibiti nayo.
Kama wewe siyo mfanyaji mkuu wa maamuzi au soko linaamua vitu vingi, usiweke fedha ambayo huwezi kuipoteza.
Na fedha ya kuuza kiwanja ni ambayo huwezi kuipoteza, labda kama unavyo viwanja vingi.

Jibu ni ndiyo kama tayari upo kwenye biashara na una uzoefu mzuri na biashara hiyo.
Tayari unaijua vizuri biashara na umeona fursa ambayo ukiongeza mtaji utaweza kutengeneza faida kubwa zaidi.

Hapo unapiga hesabu zako vizuri kiasi kwamba kuuza kiwanja chako kunakupa fursa ya kuweza kununua viwanja vingine vingi baadaye.

Biashara ni mchezo wenye kanuni na taratibu zake.
Mchezo wowote ni rahisi ukiuangalia kwa nje.
Ila unapoingia ndani ndiyo unaona vitu ambavyo hukuwa unaona.

Japo huwezi kuondoa kila hatari ya biashara, uzoefu unapunguza sana hatari ya kupoteza mtaji.

Hivyo kwa kuanza biashara, pambana kwanza kujenga mtaji wako mwenyewe kupitia kufanya shughuli nyingine au kuanza biashara isiyohitaji mtaji.

Soma; Biashara Tano Unazoweza Kuanza Kufanya Mwaka 2017 Kwa Mtaji Kidogo Au Bila Ya Mtaji Kabisa.

Halafu ukishajenya uzoefu wa kutosha,  ndipo unaweza kutumia vyanzo vingine vya mtaji ili kukua zaidi.

Kujifunza zaidi kuhusu misingi ya biashara, kupata wazo bora na kukusanya mtaji, soma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA.

Kujifunza jinsi ya kujiwekea akiba ili kujenga mtaji wa biashara, soma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA.

Na kama upo kwenye ajira ila unataka kuanza biashara kabla hujaachana na ajira hiyo, soma kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA.

Kupata vitabu hivyo wasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa vitabu popote ulipo.

Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.
http://www.somavitabu.co.tz