#SheriaYaLeo (92/366); Usimzidi Bosi Wako.

Sisi binadamu huwa tuna tabia ya wivu na kutokujiamini.
Pale mtu mwingine anapofanya vizuri kuliko sisi tunaona anapata fursa nyingi na nzuri zaidi.

Unapojihusisha na watu wengine, hupaswi kujali sana kuhusu hilo, wewe pambana kuwa bora na kuzalisha matokeo makubwa.

Lakini inapokuja kwa bosi wako, kama umeajiriwa au unafanya kazi chini ya mtu mwingine, lazima uwe makini sana.
Kwani pale unapofanya kwa ubora na viwango vya juu kuliko yeye, unaibua hisia za wivu na kutokujiamini kwake.

Ghafla anaona ni kama unawinda cheo chake na hapo atafanya kila namna kukukwamisha au hata kukuondoa kwenye nafasi yako ili usiwe hatari kwake.

Hivyo kanuni muhimu sana ya madaraka ni kamwe usimzidi aliye juu yako.
Kama ikitokea unauwezo mkubwa kuliko aliye juu yako, onyesha kwamba unayofanya ni kutokana na ushauri wake au mwongozo wake.

Yote unayofanya yaonyeshe kwamba ni matunda yake.
Kila kizuri unachokamilisha onyesha bila yeye kisingewezekana.
Kwa njia hiyo aliye juu yako anajisikia salama na hivyo kukuacha uendelee na mambo yako.
Hilo litakupa fursa ya kuendelea kujijenga na kufikia malengo yako.

Mara zote kumbuka unajihusisha na binadamu, na binadamu ni viumbe wa kihisia kuliko mantiki.
Usiangalie tu mantiki ya kile unachofanya, bali pia angalia namna gani unagusa hisia za wengine.
Na kwa walio juu yako, wafanye wajisilie vizuri na salama kupitia uwepo wako, la sivyo watafanya kila namna kukuondoa.

Haijalishi unafanya kitu kizuri na chenye manufaa kiasi gani, kama walio juu yako watajiona wapo hatarini kwa uwepo wako, hutapata fursa ya kuendelea kufanya kile unachofanya.
Lengo lako ni kupata fursa ya kuendelea kufanya kile unachofanya, hivyo waridhishe wale walio juu yako ili wakuache uendelee kufanya.
Na unawaridhisha kwa kuwafanya wajione wako juu zaidi na wewe uko chini yao.

Sheria ya leo; Mara zote wafanye wale walio juu yako wajisikie fahari kwamba wapo juu na usionekane kuwa hatari kwenye nafasi zao. Kamwe usimzidi aliye juu yako kama bado unataka kubaki kwenye kile unachofanya.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbumifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji