#SheriaYaLeo (93/366); Mfanye bosi wako ajione yuko juu zaidi.
Katika kujenga ubobezi na kufanya makubwa, kuna watu ambao wako juu yako, ambao wana nguvu fulani kwenye hatua unazotaka kupiga.
Kitendo tu cha wewe kufanya makubwa, kinawaweka wao kwenye hatari, kwa kuwafanya wajione hawana umuhimu kwako.
Hilo litaibua hisia mbaya kwao na kuwafanya wakuwekee vikwazo mbalimbali.
Kwenye sheria iliyopita tumejifunza kutokumzidi bosi wako.
Lakini hiyo pekee haitoshi, bali unapaswa kwenda zaidi ya hapo, kumfanya ajione yuko juu zaidi.
Unaweza kufanya hilo kupitia kumzawadia matokeo unayotapata ili aone yeye ni sehemu kuu ya matokeo hayo.
Unampa sifa mbalimbali kulingana na yale unayofanya na matokeo unayopata.
Hufanyi hivyo kwa maigizo tu, bali ukimaanisha kweli kutoka ndani yako.
Na hii siyo kujipendekeza wala kuwa mnafiki, bali ni kwenda na binadamu jinsi walivyo.
Ukaidi kwenye hili utakufanya ujikoseshe fursa kubwa na nzuri.
Hakuna unachopoteza kwa kumfanya aliye juu yako kujiona yuko juu zaidi.
Unachotaka wewe ni kufikia ubobezi na kufanya makubwa, usiruhusu chochote kiwe kikwazo kwako.
Sheria ya leo; Haitoshi tu kutokumzidi bosi wako, bali pia unapaswa kumfanya ajione yuko juu zaidi. Hivyo tumia matokeo ya kazi yako kumweka juu zaidi, hilo litamfanya akupe fursa nzuri zaidi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji