2591; Hakuna jipya.

Sisi binadamu wakati mwingine huwa tunashangaza sana.

Tunapenda kufanya vitu kwa mazoea, lakini inapokuja kwenye kufanikiwa, tunapenda vitu vipya vipya.

Kufanya kitu kile kile kwa kurudia rudia na kwa muda mrefu huwa inawachosha wengi.

Wanakimbilia kutafuta vitu vipya vya kufanya, ambavyo vinawasisikua kwa upya wake, lakini haviwi na manufaa yoyote kwao.

Hata kwenye kujifunza, hasa kuhusu mafanikio, wengi hujiambia hakuna jipya, mafunzo ni yale yale.

Na hiyo ni kweli kabisa, hakuna jipya, ila je hayo hayo umeshayabobea na kuweza kuyatawala vizuri?

Maana shida kubwa siyo upya au uzamani wa kitu, shida kubwa ni namna ya kutumia kila kitu ili kuweza kupata kile unachotaka.

Kama ambavyo nimekuwa nakushauri, angalia mchakato na kisha kaa kwenye mchakato.
Usiwe kama wengine ambao kila wakati wanakimbizana na vitu vipya, badala yake jua mchakato sahihi kwako na kaa kwenye mchakato huo.

Huwa inachukua muda mpaka kweli upate matokeo unayoyataka.
Kuhangaika na mapya hakuyarahisishi matokeo hayo, bali kunazidi kukuchelewesha.

Hatua ya kuchukua;
Jua mchakato sahihi kwako kufika kule unakotaka kufika, kisha weka juhudi kubwa kwenye mchakato huo. Acha kukimbizana na mambo mapya kila wakati, yatakuchelewesha sana.

Tafakari;
Mara nyingi kile kinachokufanya ujisikie vizuri huwa hakileti matokeo makubwa. Na kinacholeta matokeo makubwa siyo kinachokufanya ujisikie vizuri. Chagua unataka kujisikia vizuri au unataka kuzalisha matokeo makubwa?

Kocha.