2596; Ushindi wa kijinga.
Mtu amekukanyaga na wewe ukaamua kumkanyaga ili kulipa hilo. Swali ni je kumkanyaga kwako kumesaidia kumefuta kukukanyaga kwake?
Mtu amekutukana na wewe ukamtukana. Je tusi lako limefuta tusi lake?
Mbwa amekubwekea na wewe ukambwekea. Nani ataonekana ana tatizo hapo?
Sisi binadamu huwa tunapenda ushindi kwenye maisha.
Haijalishi ni ushindi wa aina gani, chochote kinachoashiria ushindi kwetu, tunakifanya na kukithamini.
Kwa wale ambao hawana makubwa wanayofanya kwenye maisha yao na hivyo kukosa ushindi wa maana, huwa wanatengeneza ushindi wa kijinga.
Ndipo sasa unakutana na mtu anayelipa mambo ya hovyo, yasiyo na maana yoyote kwake, ila tu yanamfanya ajione mshindi.
Wengine huenda mbali zaidi na kujihusisha na ushindi wa watu wengine. Mfano mtu kujimilikisha ushindi wa timu inaposhinda. Au kutumia ushindi wa wengine kama ni wake.
Kuhangaika na ushindi wa kijinga ni kiashiria kwamba huna ushindi mkubwa unaoendelea kwenye maisha yako.
Maana unapokuwa na ushindi mkubwa, unapokuwa na malengo unayoyafanyia kazi kwa juhudi kubwa, hatua unazokuwa unapiga ni ushindi mkubwa kwako.
Pambana na ushindi mkubwa na muhimu kwenye maisha yako ili uache kuhangaika na ushindi wa kijinga.
Hatua za kuchukua;
Itathmini kila siku yako na uone kama unafanyia kazi ushindi wa maana (malengo yako) au ushindi wa kijinga (chochote nje ya malengo yako).
Kila wakati jikite kwenye malengo yako. Ukijiona unahangaika sana na ushindi wa kijinga, jua uko nje ya malengo yako.
Tafakari;
Tatizo la mbio za panya ni kwamba hata ukishinda unabaki kuwa panya. Acha kuhangaika na ushindi wa kijinga, hata ukiupata haubadili chochote kwenye hali na maisha yako. Ni ushindi wa malengo yako ndiyo unaoleta mabadiliko ya kweli kwako.
Kocha.