2597; Ubaya wa vitu vizuri.

Huwa kuna kauli inasema kila kitu kizuri kwenye maisha huwa kinyume na sheria, hakiendani na maadili au siyo kizuri kiafya.

Na hiyo ni kwa sababu moja kubwa, sisi binadamu huwa tuna tabia ya kufanya vitu kupitiliza.
Kitu kinapokuwa kizuri au kitamu, basi tunashindwa kujidhibiti katika kukifanya au kukitumia.

Na hilo ndiyo linakuwa chanzo cha matatizo yote.
Maana kitu chochote kile kinapofanywa kwa kupitiliza, kinageuka kuwa kibaya.

Chukua mfano wa sukari.
Kwa kiwango kidogo ni muhimu kwenye mwili.
Lakini inapotumiwa kwa kupitiliza inakuwa sumu kwenye mwili.
Kupelekea watu kuwa na uzito uliopitiliza na magonjwa mbalimbali.

Kwa kija kitu kwenye maisha, hata ambacho ni kizuri, kinapofanywa au kutumiwa kwa kupitiliza, kinageuka kuwa kibaya.

Na hilo ndiyo linapelekea watu kuanguka pale wanapofanikiwa.
Maana kabla hawajafanikiwa wanakuwa hawana fursa ya kupata kila wanachotaka, hivyo mazingira yanawabana.
Lakini wanapofanikiwa na kuwa na uhuru na ziada ya kila kitu, ndipo wanashindwa kujidhibiti na kufanya mambo yanayoishia kuwaangusha.

Hatua ya kuchukua;
Siyo kwa sababu kitu ni kizuri basi ukifanye kwa kupitiliza.
Kiasi ni muhimu kwenye kila eneo la maisha.
Chagua kuwa na kiasi kwenye kila unachofanya ili mafanikio unayoyapata yaweze kudumu kwa muda mrefu.

Tafakari;
Kukosa kiasi ndiyo chanzo cha anguko la wengi baada ya kufanikiwa.
Usiruhusu hali ya kukosa kiasi ikutawale.

Kocha.