#SheriaYaLeo (104/366); Bora kushambuliwa kuliko kupuuzwa.
Kwenye safari yako ya mafanikio, unapaswa kujijengea sifa fulani ambazo zinakutofautisha na watu wengine.
Ujiwekee viwango ambavyo kila wakati utajisukuma kujifikia.
Hilo unapaswa kuliweka wazi kwa watu wote, ili wajue unasimamia upande upi na wategemee nini kwako.
Kufanya hivyo kutawafanya baadhi ya watu wasifurahishwe na sifa au viwango vyako.
Na hivyo wataanza kukushambulia, kwa kukukosoa na kuonyesha nyakati ambazo hujasimamia viwango vyako na hivyo kukuita mnafiki.
Kibinadamu unaweza usifurahishwe na hilo, hivyo ukafanya kila namna ili kuepuka usishambuliwe na wengine.
Kuepuka kushambuliwa haitakuwa na msaada kwako.
Ni bora kushambuliwa, kukosolewa na kupingwa kuliko kupuuzwa.
Maana unapopuuzwa hakuna yeyote anayejua kuhusu wewe.
Lakini unaposhambuliwa, wanaokushambulia ni kama wanakutangaza na hivyo walio sahihi kwako wanakujua.
Huwezi kukubalika na kila mtu, hata ufanye mazuri kiasi gani.
Hivyo badala ya kujificha ili watu wasikushambulie, toka hadharani na kile unachosimamia na waache wanaokushambulia wakutangaze zaidi.
Sheria ya leo; Kwa namna yoyote watu wanakuzungumzia, iwe kwa uzuri au ubaya ina manufaa kwako, kunakupa nguvu na mamlaka. Kupuuzwa ni sumu kubwa, hakuna atakayejua chochote kuhusu wewe.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji