Rafiki yangu mpendwa,
Kama nguvu yenye uwezo wa kukupa chochote unachotaka ingekutokea sasa na kuuliza kitu gani kimoja ukikipata mwaka 2022 utakuwa wa mafanikio makubwa kwako, ungejibu nini?
Hebu fikiria kwa kina na ujipe majibu ya swali hilo.
Najua wakati mwaka unaanza ulijiwekea malengo na mipango mbalimbali.
Najua siku za mwanzo wa mwaka uliweka juhudi mbalimbali katika kufanyia kazi malengo hayo.
Lakini la kutokea likatokea na sasa umeshaachana kabisa na malengo uliyoyaweka kwa shauku na hamasa kubwa.
Sasa leo naleta kwako nguvu yenye uwezo wa kukupa chochote unachotaka kwa mwaka huu 2022.
Chochote kile, ila sharti ni hili, kiwe kitu kimoja tu.

Hivyo ni kitu gani kimoja ambacho ukikifanya au kukipata mwaka huu 2022 utauhesabu kuwa wa mafanikio kwako?
Kwa chochote ambacho umechagua, nataka nikushirikishe jinsi nguvu hiyo inaweza kukupatia kitu hicho.
Nguvu hiyo ni kufanya kitu hicho kila siku bila ya kuacha hata siku moja.
Haijalishi unakifanya kwa udogo kiasi gani, wewe kifanye kila siku.
Angalia mifano hii;
1. Lengo lako ni kuweka akiba zaidi ili uweze kukamilisha kipango yako muhimu.
Chagua kuweka akiba ya elfu 1 tu kila siku bila kuacha hata siku moja. Kama unasoma hapa, huwezi kukosa elfu moja kwa siku. Unaweza kuidharau elfu moja, lakini ikusanye kila siku na utaona maajabu yake.
Hivyo chagua kuacha chochote kitakachokupa elfu moja kila siku, acha kunywa soda, au bia, au punguza mlo mmoja au tembea kwa miguu badala ya daladala au tumia daladala badala ya gari au acha kununua vocha.
Yote hayo ukifanya hutakufa na utajihakikishia elfu moja au zaidi ya kuweka akiba kila siku.
2. Lengo lako ni kuongeza kipato chako zaidi.
Chagua kuongeza masaa mawili kila siku kwenye kazi au biashara yako.
Wahi mapema kwa saa moja kabla ya muda uliozoea na chelewa kumaliza au kufunga kwa saa moja zaidi.
Kila siku fanya jukumu la ziada au tafuta mteja mmoja mpya.
Fanya hayo kila siku na utashangaa jinsi kipato chako kitakavyokuwa kinaongezeka.
3. Lengo lako ni kusoma na/au kuandika zaidi.
Chagua kutenga muda wa kusoma na/au kuandika kila siku bila kuacha.
Kusoma chagua kurasa kumi tu kila siku na andika uliyojifunza.
Kuandika chagua kuandika maneno 250 tu kila siku bila kuacha hata siku moja.
Fanya hivyo na mwaka utakuwa bora na wa kipekee sana kwako.
Rafiki, umeona hapo kwamba nguvu ya kupata chochote unachotaka ni kufanya kila siku bila kuacha.
Lakini kusema ni rahisi, kufanya ni kugumu.
Unaweza kuwa umekubaliana na mimi hapo juu na ukawa umepata hamasa sana na siku chache ukafanya kweli.
Lakini kama ilivyokuwa kwenye malengo ya mwaka mpya, hutaendelea kwa muda mrefu, utaishia njiani.
Ni kwa kuona hilo nimekuandalia mfumo rahisi wa uwajibikaji utakaokusukuma uendelee kufanya kila siku bila kuacha.
Nakukaribisha kwenye CHANGAMOTO YA SIKU 100 za kufanya kitu kimoja bila kuacha hata siku moja.
Changamoto hiyo inafanyika kupitia kundi maalumu la wasap ambapo unajiunga na kufanya yafuatayo;
1. Kujitambulisha.
2. Kueleza nini unapanga kufanya kila siku na ushahidi utakaoweka kwenye kundi kwamba umefanya.
3. Kufanya kila siku na kuweka ushahidi.
Ukishindwa kutekeleza hayo, unajiondoa mwenyewe kwenye kundi hilo.
Mwisho wa kujiunga na kundi hilo ni jumapili tarehe 13/02/2022.
Siku ya jumatatu tarehe 14/02/2022 itakuwa ya kujitambulisha na kueleza unachofanyia kazi na ushahudi utakaoweka.
Siku ya jumanne tarehe 15/02/2022 itakuwa ndiyo ya kuanza rasmi kwa changamoto.
Karibu sana utumie fursa hii kuufanya mwaka 2022 uwe wa mafanikio makubwa kwako.
Jiunge na kundi hilo la changamoto kwa kutumia kiungo hiki; https://chat.whatsapp.com/G91eD4TykPT8PjM1wyNukX
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.