2602; Udhaifu wa watu.

Sisi kama binadamu kwa ujumla, huwa tuna madhaifu yetu mengi.

Mfano kushindwa kufikiri kwa usahihi pale hisia zinapokuwa kali.

Au hitaji la kuwa ndani ya kundi na hivyo kufuata mkumbo.
Na kwa kufuata mkumbo, mtu anaweza kufanya vitu ambavyo peke yake asingekuwa tayari kufanya.

Kuna watu wamekuwa wanatumia madhaifu hayo ya binadamu kujinufaisha kwa namna mbalimbali.

Kwenye biashara madhaifu ya binadamu yamekuwa yanatumika sana kuwashawishi watu kununua, hata kama vitu havina manufaa kwao.

Pia kwenye siasa madhaifu ya binadamu yamekuwa yanatumika sana na viongozi kupata kile wanachotaka, hata kama hakina manufaa kwa wengi.

Inashawishi sana kutumia madhaifu ya binadamu kupata kila unachotaka, lakini ni njia ya mkato ambayo huwa haidumu.
Mwisho njia hiyo hukosa nguvu na mtu kuishia kushindwa vibaya.

Hatua ya kuchukua;
Madhaifu ya binadamu yataendelea kuwepo. Kama itabidi uyatumie, basi hakikisha ni kitu chenye manufaa kwa watu unaowalenga na siyo chenye manufaa kwako tu.
Epuka sana njia za mkato kwenye jambo lolote lile, maana zinaishia kukuacha na mikato mingi.

Tafakari;
Kupata unachotaka kwa gharama zozote zile ni lengo zuri. Lakini pale gharama hizo zinapokuwa ni maumivu kwa wengine mwisho wake huwa mbaya kwako.

Kocha.