2609; Asili haipendi utupu.
Kama kuna kitu ambacho asili huwa haikipendi kabisa ni utupu.
Safisha chumba chako vizuri kisha kifunge na kuondoka.
Ukirudi utakuta kuna vitu vimejikusanya, vumbi, utando wa wadudu na vingine.
Lima shamba lako na usipande chochote na haitachukua muda magugu mbalimbali yatakuwa yameota kwenye shamba hilo.
Usipofanya juhudi za makusudi za kuweka kile unachokitaka mahali penye utupu, asili itapajaza kwa vitu visivyokuwa na umuhimu.
Kama hutaamua kuwa na fikra sahihi kwako, akili yako itajazwa fikra zisizo sahihi kutoka kwa wengine na vyombo vya habari.
Kama hutaamua kujenga tabia sahihi kwako, utajikuta umejenga tabia zisizo sahihi ambazo zitakuwa kikwazo kikubwa kwako.
Kama hutaweka juhudi kwenye kujenga mahusiano bora na yenye manufaa kwako utajikuta upo kwenye mahusiano ambayo siyo mazuri.
Kwa hakika, kila kitu kizuri kinahitaji kujengwa kwa makusudi, juhudi kubwa ziende kwenye hilo.
Kama juhudi za makusudi hazitawekwa, basi asili itaweka kisichokuwa bora.
Mazoea yatatengeneza yenyewe kitu cha kujaza hapo.
Na hayo huwa siyo mazuri.
Hatua ya kuchukua;
Tathmini kila eneo la maisha yako na jiulize kama umelitengeneza kwa makusudi au limetokea lenyewe kwa mazoea.
Kwa kila ambacho hujajenga mwenyewe, jua hakiwezi kuwa bora kwako.
Hivyo anza kujenga mwenyewe kila eneo la maisha yako ili uweze kuwa na maisha unayoyataka.
Tafakari;
Upo vile ulivyo sasa kutokana na jinsi uliyojijenga huko nyuma.
Kama unataka kuwa tofauti na ulivyo sasa, lazima uchague kujijenga kitofati. Hilo linahitaji juhudi kubwa ili kulifanikisha, kuwa tayari kuweka juhudi hizo.
Kocha.