2610; Jenga.
Kila kitu tunachonufaika nacho leo hapa duniani ni kwa sababu watu walichukua hatua ya kukijenga.
Chakula, mavazi, nyumba, magari na mengine yote, ni matokeo ya watu kujenga.
Watu walioweza kujenga yote tunayofurahia sasa, walikuwa na maono makubwa ambayo wengine hawakuamini yangewezekana.
Laki kwa kujiamini na kufanyia kazi, mwishowe waliweza kujenga vitu vyenye manufaa makubwa.
Watu wote waliopata mafanikio makubwa kwenye maisha yao ni wajengaji.
Mafanikio hayaji kwa maneno tu au kuamini tu inawezekana.
Bali mafanikio yanatokana na kile ambacho mtu anajenga.
Na kadiri kinavyokuwa kikubwa na chenye manufaa kwa wengi, ndivyo mafanikio yanavyokuwa makubwa.
Uzuri ni kwamba kila mtu anao uwezo wa kujenga. Iwe ni biashara, kazi, mahusiano, uwekezaji, sifa binafsi n.k. Vyote hivyo ni vitu vyenye manufaa pale vinapojengwa vizuri.
Hatua ya kuchukua;
Kila mara jiulize na kujijibu ni vitu gani unajenga kwenye maisha yako? Pamoja na vingi unavyoendelea kujenga, kuna vitatu ambavyo vinahitaji nguvu zako kubwa; biashara, uwekezaji na ubobezi.
Jenga biashara inayoweza kujiendesha yenyewe bila kukutegemea.
Jenga uwekezaji unaokua thamani na kukulipa gawio linalotosha kuendesha maisha bila ya kutegemea kufanya kazi.
Na jenga ubobezi mkubwa unaokuwezesha kuacha alama hapa duniani.
Tafakari;
Kama hujengi basi unabomoa.
Weka juhudi za makusudi kwenye kujenga ili uepuke kubomoa yale yenye manufaa kwako.
Kocha.