#UkurasaWaLeo (114/366); Waepuke wenye kisirani.
Kuna watu mbalimbali ambao wamepitia magumu na kushindwa kwenye maisha.
Huwa tunasukumwa kuwaonea huruma watu hao na kuchukua hatua mbalimbali kuwasaidia.
Lakini siyo wote wanaofaa kusaidia.
Wapo ambao magumu na kushindwa wanakopitia wanakuwa wamejitakia wenyewe.
Hao ni watu wenye kisirani na mikosi ambao kwa tabia zao wenyewe wamejiingiza kwenye matatizo ya kujitakia.
Unapojaribu kuwasaidia watu wa aina hii, huwa hawabadiliki.
Lakini mbaya zaidi wanakuingiza wewe kwenye kisirani na mikosi waliyonayo.
Matatizo yao yanakuwa matatizo yako na yanakusumbua na kupelekea kushindwa vibaya.
Haimaanishi usiwasaidie wenye matatizo, ila angalia kwanza unayemsaidia, asije akakuzamisha na wewe.
Unaweza kuwajua watu wenye kisirani kwa kuangalia maisha yao ya nyuma.
Angalia matatizo mbalimbali waliyopitia ambayo ni ya kujisababishia.
Angalia mahusiano yao mengi ambayo yamevunjika.
Angalia kazi na biashara nyingi ambazo wamefanya na kuishia kushindwa.
Na pia angalia jinsi wanavyowalaumu wengine kwa yote waliyopitia kwenye maisha yao.
Kwa bahati mbaya sana watu wenye kisirani huwa na ushawishi mkubwa na wakikueleza mambo yao ni rahisi sana kuingiwa huruma na kuona wanahitaji sana msaada wako.
Na hapo ndipo unapopaswa kuwa na tahadhari kubwa, kwani huendi kuwasaidia, bali na wewe unaenda kuanguka.
Ukishagundua mtu ana kisirani na mikosi, kaa naye mbali.
Muonee huruma utakavyo, lakini kamwe usijihusishe na mambo yake.
Kwani utaishia kuanguka na kushindwa kama yeye.
Huku ukiwa hujawabadili kwa namna yoyote ile.
Hivyo ndivyo wenye kisirani walivyo, hakuna namna unaweza kuwasaidia.
Sheria ya leo; Wakati mwingine watu wanajiingiza wenyewe kwenye mikosi, unapojihusisha nao, wanakuingiza kwenye mikosi hiyo pia. Waepuke sana watu wa aina hiyo, kwani huwezi kuwasaidia na wanaishia kukuangusha.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji