2611; Maoni ya wengine.
Mstoa Marcus Aurelius amewahi kunukuliwa akisema, kila mtu anajipenda na kujiheshimu, lakini anaishia kuyapa maoni ya wengine uzito kuliko maoni yake binafsi.
Wengi tunasahau kwamba maoni siyo ukweli au uhalisia. Bali ni kile ambacho watu wanafikiria kwa wakati huo, ambacho pia ni rahisi sana kunadilika baada ya muda.
Kitendo cha maoni ya watu kubadilika kwenye kitu kile kile kinapaswa kukufanya uone ni jinsi gani maoni siyo ukweli na hivyo hupaswi kuyapa nguvu kubwa.
Pamoja na maoni kwa ujumla wake kuwa na changamoto, kuna ya aina mbili ambayo unapaswa kuyaepuka kama ukoma.
Moja ni maoni yanayotolewa na watu wasiokuwa sahihi.
Hapa ni mtu asiye na uzoefu wowote na asiyeelewa hali yako kwa undani anapokimbilia kukupa maoni kwa kile alichoona au kusikia kutoka kwako.
Hayawezi kuwa maoni sahihi kwa namna yoyote ile, hivyo yapuuze.
Hapa pia yanaingia maoni ya wale ambao hawajaingia gharama yoyote, haya tuyaite maoni ya bure.
Mfano unafanya biashara, kisha mtu ambaye hajawahi kutoa fedha kununua unachouza akawa anakupa maoni.
Hayo ni ya kuepuka kama ukoma, siyo ya kweli na hayana manufaa yoyote kwako.
Kama mtu hajatoa fedha yake akanunua unachouza, maoni yake juu ya kitu hicho hayana maana wala msaada wowote kwako.
Mbili ni maoni yanayotolewa kwenye kitu ambacho huwezi kukibadili tena.
Hapa mtu anakupa maoni yake kwenye maamuzi ambayo tayari umeshayafanya na huwezi kuyabadili.
Mfano umeshajenga nyumba halafu mtu anakupa maoni yake kwenye ramani ya nyumba hiyo.
Au umeshafunga ndoa halafu mtu anakupa maoni yake juu ya mwenza wako.
Hata kama yatakuwa mazuri kiasi gani, hayana msaada kwako, hivyo yataishia tu kukuumiza kwa kuwa huna cha kufanya.
Ukishafanya maamuzi ambayo huna mpango au huwezi kuyabadili, funga kabisa kupokea maoni ya watu juu ya hilo.
Tatizo la maoni ni kwamba yanatokana na hisia zaidi kuliko mantiki.
Na kwa sababu wakati mwingine ni vigumu mtu kuelezea hisia zake, anaishia kusema yasiyokuwa sahihi.
Hivyo maoni mengi ni ya kuyaepuka na kuyapuuza, kwa sababu siyo kweli na hayana manufaa kwako.
Japo kuna maoni unapaswa kuyazingatia, hasa yale yanayotoka kwa wataalamu wa eneo husika na wale wanaokujua vizuri.
Lakini hata hayo ni ya kuzingatia, siyo kwamba ndiyo sheria ambayo lazima uifuate.
Hatua ya kuchukua;
Kila wakati jikumbushe maoni siyo ukweli, ni mawazo ambayo watu wanayo kulingana na hisia walizonazo kwa wakati huo. Hisia zao zilibadilika na maoni hayo yanabadilika.
Hivyo mara zote kazana kuujua ukweli ili uutumie kufanya maamuzi sahihi.
Na kwa upende wa pili, epuka sana kuwa na maoni kwenye kila kitu. Maoni mengi unayokuwa nayo siyo sahihi, hivyo usione una umuhimu sana wa kuwa na maoni na kuyatoa kwa kila mtu.
Tafakari;
Maoni ni rahisi na yanaweza kubembeleza kadiri mtu anavyotaka.
Ukweli ni mgumu na haubembelezi.
Kazana kuufikia ukweli na achana na maoni.
Maamuzi unayofanya kwa kutumia ukweli hubaki kuwa maamuzi bora.
Maamuzi unayofanya kwa kutumia maoni hayana uhakika wa kuwa bora, ni kama kubahatisha hivi.
Kocha.
Asante sana Dr Amani kwa hili.Huu ukurasa umeingia mpaka Moyoni kwangu.
LikeLike
Karibu.
LikeLike