#SheriaYaLeo (121/366); Usionekane mkamilifu sana.

Unapokuwa kwenye eneo au kundi ambalo unashirikiana na wengine ili uweze kupata mafanikio unayoyataka, kuonekana mkamilifu sana ni kikwazo kikubwa kwako.

Kadiri unavyoonyesha uwezo wako mkubwa na usivyokuwa na mapungufu, ndivyo wengi wanavyojenga wivu na chuki juu yako.

Unaweza kudhani kuonyesha uwezo na ukamilifu wako kunafanya watu wakukubali zaidi.
Lakini pale mnapokuwa kwenye mazingira ya wengi kutaka nafasi moja, uwezo wako mkubwa unawafanya wengine wakuone ni hatari kwao.

Hivyo watafanya kila namna kuhakikisha wanakuangusha. Watatafuta kila sababu ya kukukwamisha lakini hawatakuambia sababu kamili ambayo ni ukamilifu wako unaowafanya wajione kuwa hatarini.

Ili kuondokana na changamoto hiyo, unahitaji kuficha sehemu ya uwezo wako mkubwa.
Mara kwa mara fanya vitu vinavyoashiria una udhaifu kwenye maeneo fulani ili wale wanaokuzunguka wakuone ni kama wao na hivyo kutokuwa hatari sana kwao.

Hakikisha uwepo wako baina ya wengine hauonekani hatari kwao. Lakini ndani yako endelea na mikakati ya kukupa kile unachotaka au kukufikisha unakotaka.

Hili ni muhimu sana kwenye nafasi za uongozi au kazi, usipolizingatia utawekewa vikwazo vya kila aina na wale wanaoona unakuwa hatari kwao.

Sheria ya leo; Kuonekana bora kabisa kuliko wengine ni hatari kwako. Lakini hatari kubwa zaidi ni kuonekana huna madhaifu au makosa yoyote. Wivu hutengeneza maadui wengi wa kimya ambao hufanya kila namna kukuangusha. Ondokana nao kwa kutokuonekana mkamilifu sana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji