2618; Unayapenda mafanikio, ila hayakupendi.

Wakati naanza huduma hii ya mafunzo, ushauri na ukocha wa mafanikio, nilikuwa naamini kila mtu anawesa kufanikiwa.

Kwamba mtu akishakuwa tu na nia ya kufanikiwa, akapata maarifa na miongozo sahihi, basi hakuna namna atashindwa kufanikiwa.

Kadiri ninavyoendelea kufanya kazi kwa ukaribu kabisa na walio wengi, nazidi kuona jinsi mtazamo niliokuwa nao awali haukuwa sahihi.

Naona wazi kabisa kwamba kuna watu wanayapenda sana mafanikio, ila mafanikio hayawapendi.

Wengi wanaeleza kabisa mafanikio wanayotaka kufikia, ndoto kubwa walizonazo na wapo tayari kuamini na kuwa chanya kwamba watazifikia.

Ila sasa hawafikii ndoto hizo na wala hawafanikiwi, licha ya kupambana na kuhangaika sana.

Hawafanikiwi siyo kwa sababu mafanikio hayawezekani.
Ila ni kwa jinsi walivyo, wanakuwa kinyume kabisa na mafanikio.
Ni kama wanapishana na gari la fedha, wao wanaenda upande huu, fedha zinaenda upande tofauti.

Kinachotokea ni tabia ambazo mtu tayari anakuwa nazo zinakuwa kikwazo kikubwa kwake kufanikiwa.
Licha ha juhudi kubwa ambazo mtu anakuwa anaweka, tabia zake zinakuwa kikwazo kwake kupata mafanikio.

Hii haimaanishi kwamba hakuna tena namna ya kufanikiwa kwa walio wengi.
Bali inamaanisha kuna kazi kubwa ya kuvunja tabia ambazo zimekuwa kikwazo.

Na hakuna kitu kigumu kuvunja kwenye maisha kama tabia.
Ni sawa na kujiua wewe wa zamani ili uzaliwe mwingine mpya.
Bila ya kupitia zoezi hilo, utaishia kuyapenda mafanikio, ila yenyewe hayatakupenda kamwe, kwa kuwa huendani nayo.

Hatua ya kuchukua;
Pima mapenzi yako kwenye mafanikio, juhudi ambazo umekuea unaweka na hatua ambazo umepiga mpaka sasa.
Kama hatua haziendani na juhudi na mapenzi, kuna kikwazo ambacho kinaanzia ndani yako.
Bila kivuka kikwazo hicho, mafanikio yataishia kuwa hadithi.
Vunja vikwazo vyote vinavyokuzuia kufanikiwa, ambavyo vinaanzia kwenye tabia ambazo tayari umejijengea.

Tafakari;
Kwenye kila jamii wanaofanikiwa ni wachache na wanaoshindwa ni wengi.
Unaweza kuona kama ni njama imepangwa, kwamba wachache wafanikiwe na wengi washindwe.
Lakini siyo, wachache sana ndiyo walio tayari kujitoa kwa viwango ambavyo mafanikio yanataka mtu ajitoe.
Walio wengi wanayapenda tu mafanikio, ila hawapo tayari kujitoa kwa namna mafanikio yanavyowataka wajitoe.

Kocha.