#SheriaYaLeo (123/366); Wakabili wanaocheza rafu.

Katika safari ya mafanikio na maisha kwa ujumla, utakutana na watu ambao wanacheza rafu.
Hawa ni wale ambao wapo tayari kutumia kila namna kupata kile wanachotaka.

Kwa nje watu hao hujionyesha ni wema, wastaarabu na wanaojali.
Ila kwa ndani watu hao ni sumu, wenye mbinu na hila za kukunasa kwenye mitego mbalimbali ili watimize azima yao.

Utawajua watu hao kwa namna watakavyojiaminisha kwako ni watu wema na ukawaamini haraka.
Halafu ghafla wanabadilika na kukupa mashinikizo mbalimbali baada ya kuwa wamekunasa mahali ambapo siyo rahisi kutoka.

Ukishaingia kwenye anga za watu wa aina hii ni vigumu kutoka ukiwa salama.
Hivyo njia bora ni kuwaepuka kabla hujanasa kwenye njama zao.
Zijue mapema tabia za watu wa aina hiyo na waepuke haraka.
Usikubali wakushawishi kwa namna yoyote ile.
Usiwaamini kwa vyovyote wanavyokuaminisha.
Jua hiyo yote ni mitego ya kukunasa ili wakutumie kupata wanachotaka.

Utawatambua watu hao mapema kupitia tamaa waliyonayo ya kupata wanachotaka na utayari wa kufanya chochote, hata kisichokuwa sahihi ili kupata wanachotaka.
Huwa wapo tayari kutumia njia zisizo sahihi kupata wanachotaka.
Na huwa ni watu wa kujisifu sana na kuficha madhaifu yao, huku wakisema sana madhaifu ya wengine na kuwalaumu kwa namna mbalimbali.

Ukishatambua unakabiliana na mcheza rafu, huhitaji kufanya chochote zaidi ya kumpuuza na kuwa mtulivu.
Utulivu wako utamvuruga kwa kiasi kikubwa na kumsukuma kufanya mambo yatakayoonyesha tabia zake anazozificha.

Sheria ya leo; Tumia fursa hizi za kuwajua wengine kama sehemu ya ubobezi binafsi. Kadiri unavyoweza kuwatambua na kuwakabili wacheza rafu ndivyo unavyopata nguvu na kujiamini kuendelea na safari ya mafanikio, ukijua unaweza kukabiliana na chochote.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji