2619; Siyo hawamudu, bali hawajali.

Kama unauza kitu, iwe ni bidhaa au huduma na wateja uliowapata hawapo tayari kulipia, ni rahisi kuona labda hawamudu.

Utakimbilia kuona bei ndiyo kikwazo kwao, ni kubwa kwao na hivyo hawamudu.
Na wanaweza kukuambia hivyo kweli.

Lakini hata utakapojaribu kupunguza bei, bado hawatakuwa tayari kununua.
Wataendelea kukupa sababu zisizo na ukomo.

Leo nakwenda kukuambia ukweli ambao utakutikisa, ukweli mchungu, lakini ndivyo ulivyo, hakuna namna.
Ukijua ukweli huu na kuufanyia kazi, utanufaika sana.

Ukweli wenyewe ni huu; kama watu hawalipii kile unachouza, tatizo siyo kwamba hawakimudu, bali tatizo lao kuu ni kwamba hawakijali.

Rudia kusoma hiyo sentensi ili izame ndani kabisa, kwani ndiyo iliyobeba kila unachohitaji kujua kwenye safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.

Iko hivi rafiki, pale watu wanapokuwa wanakitaka kitu kweli na wanakijali sana, basi watafanya kila namna waweze kukipata.

Angalia hilo kwenye maisha yako na pia angalia kwenye maisha ya wengine.
Hakuna ulichotaka na kukijali kweli na ukawa tayari kukikosa.

Hivyo kabla hujakimbilia kupunguza bei ya kile unachouza, kwa sababu watu hawanunui, tafuta kwanza watu sahihi.
Tafuta watu wenye uhitaji wa kweli na ambao wanakijali kweli kitu hicho.
Pata watu ambao hawayaoni maisha yao yakienda bila ya kitu hicho na bei haitakuwa kikwazo kwao.

Pita njiani ukiuza boya la kuogelea na hakuna atakayekuwa tayari kununua, haijalishi utauza kwa bei ndogo kiasi gani.
Nenda baharini ukutane na mtu anayezama maji na mwonyeshe kwamba una boya, hatauliza bei, atataka umuuzie boya hilo, maana kwake hakuna maisha bila boya.

Hatua ya kuchukua;
Chukulia unachouza ni boya na hivyo wajibu wako ni kutafuta watu ambao wanazama. Watu hao hawana muda wa kuhangaika ba bei, maana kila sekunde wanayochelewa ni madhara makubwa kwao.
Mara zote usianze kukimbilia bei, jiulize kwanza kama wateja ulionao ni sahihi.
Maana bila wateja sahihi, bei haiwezi kuwa na ushawishi.

Tafakari;
Siyo kila mwenye uhitaji wa kile unachouza ni mteja sahihi kwako.
Mteja sahihi ni yule ambaye pia anajali sana kuhusu unachouza, ambaye hayaoni maisha yake yakiwezekana nje ya kile unachouza.
Ukaweza kuwapata hao kwa wingi, utaifurahia sana biashara unayofanya.

Kocha.