2621; Machache kuhusu wewe yanawatosha.
Sisi binadamu tuna kasumba moja, kadiri tunavyokijua zaidi kitu ndivyo tunavyokichukulia kawaida na kukidharau.
Lakini pale tunapokuwa hatukijui sana kitu huwa tunakiheshimu na kukichukulia kwa uzito mkubwa.
Kwa kujua hili, wawekee watu mipaka ya kujua kuhusu mambo yako.
Kadiri watu wanavyojua machache kuhusu maisha yako binafsi, ndivyo wanavyokuheshimu.
Lakini watu wanapojua mengi kugusu maisha yako binafsi, wanakuchukulia kawaida.
Hili halimaanishi kuwa msiri au kuwadanganya wengine.
Bali inamaanisha kutokuweka wazi kila kitu chako, kwa sababu hata unapoweka wazi, hakuna manufaa yoyote unayoyapata.
Wajulishe watu kwa kiasi ambacho kinatosha ili kuendeleza mahusiano yenu, lakini usiende zaidi ya hapo.
Kwa zama tunazoishi sasa, zama za mitandao ya kijamii, watu wanashawishika sana kuanika kila kitu kuhusu maisha yao binafsi.
Halafu wanashangaa pale wanapokutana na vikwazo kwenye mambo mbalimbali.
Kuanika mambo yako binafsi siyo tu kunawafanya watu wakudharau, bali pia kunaibua wivu kwa baadhi ya watu. Na wivu huo hupelekea wakukwamishe kwenye mambo mbalimbali.
Hatua ya kuchukua;
Weka mipaka kwenye taarifa ambazo watu wanakuwa nazo kuhusu maisha yako binafsi.
Kuondoa wale wa karibu, hakikisha wengine hawajui mengi kuhusu maisha yako binafsi.
Kadiri wanavyojua kwa uchache ndivyo inavyokuwa bora kwako.
Tafakari;
Rahisi haithaminiki.
Kama watu wanajua kila kitu kuhusu wewe, unakuwa rahisi kwao na hivyo hawakupi thamani kubwa.
Kocha.