2624; Kanuni ya heshima au imani.
Watu wamekuwa wanalalamika kwamba hawaheshimiwi au hawaaminiwi.
Lakini ukiangalia kwa uhalisia, tatizo huanzia kwa watu kutokujiheshimu au kujiamini wenyewe.
Leo napendekeza kanuni rahisi ambayo ukiifuata utajijengea heshima kubwa na kuaminika na wengine.
Kanuni hiyo inakwenda hivi;
Heshima/imani = utekelezaji/ahadi
Ili heshima au imani iwe juu, utekelezaji unapaswa kuwa mkubwa kulingana au kuzidi ahadi.
Kama unaahidi mengi halafu huyatekelezi, hujiheshimu na hujiamini na hapo pia unakuwa umewapa wengine sababu ya kutokukuheshimu na kukuamini.
Kama unatekeleza kila unachoahidi unajiheshimu na kujiamini na hapo wengine wanalazimika kukuheshimu na kukuamini pia.
Na kama unatekeleza zaidi ya ulivyoahidi, hapo unakuwa wa kipekee, mmoja kati ya wachache sana wanaofanya kwa utofauti. Heshima na imani kwako vinakuwa vya viwango vya juu kabisa.
Huhitaji tena kuwalazimisha wengine wakuheshimu na kukuamini, hilo litatoka kwao moja kwa moja na watapeleka sifa zako kwa wengine.
Yote haya yanaanzia ndani yako, hakuna anayekulazimisha uahidi chochote.
Hivyo ahidi na tekeleza zaidi ya ulivyoahidi.
Kwa hayo tu, utajijengea sifa, heshima na uaminifu mkubwa kwa wengine bila ya kujali nini unafanya.
Hatua ya kuchukua;
Kwa chochote kile unachoahidi, iwe ni kwako binafsi au kwa wengine, tekeleza zaidi ya ulivyoahidi.
Ifanye hii kuwa sheria yako kuu kwenye maisha na utaona mabadiliko makubwa.
Tafakari;
Kuahidi ni rahisi, kutekeleza ni ngumu.
Unapotekeleza zaidi ya unavyoahidi, unajitenga na wengi ambao hawawezi kufanya hivyo.
Haijalishi unafanya nini, kutekeleza zaidi ya ulivyoahidi ni njia ya kujitofautisha na wengine wote wanaofanya kitu hicho.
Kocha.