2629; Hawataki ushauri wako.

Nimewahi kuandika mara kadhaa kuhusu ushauri wa bure.
Nikisisitiza usimpe mtu ushauri kama hajakuomba na usipokee ushauri kwa mtu kama hujamuomba akushauri.

Pia nikaeleza jinsi ushauri wa bure ulivyo na gharama pale unapoufanyia kazi, kwa sababu unakuwa haujatolewa kulingana na uhitaji uliopo.

Leo nakwenda kukupa sababu nyingine ya kuondokana na tabia ya kutoa au kupokea ushauri wa bure.
Sababu hiyo ni watu hawataki ushauri wako. Na wewe pia hutaki ushauri wa watu.
Hasa pale ambapo ushauri hauendani na kile ambacho mtu anapendelea au anataka.

Watu wanapokuwa hawataki ushauri, huwa hawakosi sababu ya kuukosoa.
Ukiwa masikini na ukawashauri watu, watakuambia kama ushauri wako ni mzuri mbona hujaufanyia kazi ukakunufaisha.
Ukiwa tajiri na ukawashauri watu, watakuambia ni rahisi kwako kwa sababu wewe ni tajiri.
Kwa vyovyote vile watu hawakosi cha kupinga kwenye ushauri.
Hivyo epuka sana kutoa au kupokea ushauri wa bure, tena ambao hujaombwa.

Ni tabia yetu binadamu kutaka kusikia kile tunachotaka kusikia.
Tunaposikia kitu cha tofauti na tunachotaka hatuwi tayari kukifikiria kama kina manufaa.
Tunakikataa mara moja kwa sababu hatutaki mgogoro wa kifikra.

Hatua ya kuchukua;
Pale unapotaka kupata ushauri sahihi, chagua mtu sahihi kwenye kukupa ushauri huo na ili uuthamini na kuufanyia kazi, mlipe akushauri.
Na pale watu wanapokuja kwako kutaka ushauri, hakikisha ni eneo ambalo kweli una ujuzi na uzoefu wa kutosha na watoze fedha ndiyo uwashauri.

Tafakari;
Watu huwa hawathamini vitu vya bure, ikiwepo ushauri.
Hivyo kuliko utoe ushauri wa bure, ni bora ukae kimya.
Maana kwa kutoa kwako tu ushauri unaweza kukosana na watu pale unapowaambia wasichotaka kusikia.

Kocha