Rafiki yangu mpendwa,

Chombo kikubwa cha habari nchini China (Horizon News), kilichapa kwa makosa maelekezo yaliyokuwa yametolewa kwa wahariri wake.

Pamoja na mengine mengi, maelekezo hayo yaliwataka wahariri kuhakikisha hawachapishi habari yoyote inayoichafua Urusi au kusiria upande wa magharibi.

Pia walisisitizwa kudhibiti maoni yanayowekwa na wasomaji ili kuhakikisha hakuna chochote kinachoharibu upande wao kinawekwa.

Rafiki, huu ni upande mmoja wa mashariki kwenye vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine.
Kwa upande wa magharibi nao wana mikakati yao katika kuruhusu habari gani zisambae ili kutengeneza picha wanayotaka wao.

Hivyo basi, kitu bora kabisa unachoweza kufanya wakati huu wa vita ni kutokufuatilia habari yoyote.

Ndiyo, usijisumbue kabisa kufuatilia habari wakati huu wa vita.
Hiyo ni kwa sababu sehemu kubwa ya habari unazopewa siyo ukweli, bali ni propaganda zilizoandaliwa kwa makusudi maalumu.

Sehemu kubwa ya vita hii ipo kwenye propaganda zaidi.
Kila upande ukipambana kuonyesha kwamba upo sahihi kwenye hii vita.

Kama haupo eneo la tukio, ni vigumu sana ukaweza kujua hali halisi ya vita.

Watu wametumia mpaka picha za zamani kusambaza propaganda zao kuhusu vita hii.

Hivyo basi rafiki yangu, ili kupata utulivu wa akili na kupunguza msongo usio na maana, acha kufuatilia habari za hii vita.

Sisemi kwamba hakuna vita au kwamba haina madhara.
Nina hakika kuna watu wasio na hatia ambao wanakufa kila siku kutokana na vita hii.
Nina hakika familia zinavurugika, miji kubomolewa na mengine mabaya yanaendelea.

Lakini huwezi kusaidia lolote kwenye hayo kwa kufuatilia habari kwa masaa 24 kutaka kujua kila kinachoendelea kwenye hii vita.

Kwa bahati mbaya sana hii ndiyo vita kubwa inayotokea kwenye zama hizi za mitandao ya kijamii, zama ambazo watu wamekuwa na uraibu mkubwa kwenye mitandao hiyo.

Hivyo vita ya propaganda imeshamiri kwenye mitandao ya kijamii.
Kila upande ukitumia kila mbinu kusambaza propaganda zake ili kupata huruma kutoka kwa wengi.

Usikubali kutumiwa kwa namna hiyo, wewe achana na habari hizo za vita, maana hakuna unachoweza kufanya kuathiri vita hiyo.

Ufanye nini sasa kama hufuatilii habari  wakati huu wa vita?

Jibu ni moja, tumia muda huo kujifunza na kuboresha kazi au biashara unayofanya.
Hicho ndiyo kitu pekee kilicho ndani ya uwezo wako wa kuathiri.

Na kama kazi yako inahusu kufuatilia hizo habari za vita, basi jifunze namna ya kupata habari halisi na siyo propaganda.

Wakati huu wa vita uraibu wa habari na mitandao ya kijamii umekuwa mara dufu.
Hivyo ni wakati mzuri sana kwako kusoma kitabu cha EPUKA UTUMWA WA KIDIJITALI ili uweze kuondokana na mitego ya kipropaganda uliyotegewa ili kunasa huruma yako.

Jipatie nakala yako ya kitabu hiki leo kwa kuwasiliana na 0752 977 170 ili usitumike kwa manufaa ya watu wengine.

Utulivu wako ni muhimu sana katika safari ya mafanikio kwenye maisha yako.
Usiuvuruge kwa kufuatilia vitu ambavyo huna namna ya kuviathiri.
Peleka umakini wako kwenye yale unayoweza kuathiri.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.