2631; Kujieleza na kujitetea.
Ukweli huwa unabaki kuwa ukweli, uwe unatetewa au hautetewi.
Wakati mwingine ukijaribu sana kuutetea ukweli, unaanza kuonekana kama uongo.
Uongo ndiyo unahitaji maelezo mengi na kutetewa ili ukubalike na wengine.
Na uongo huwa unahitaji uongo mwingine mkubwa zaidi ili usianguke.
Mara zote jua upo upande upi, wa ukweli au wa uongo.
Ukiwa upande wa ukweli, huhitaji kujieleza au kujitetea sana, unaeleza ukweli jinsi ulivyo kisha kukaa kimya.
Ukiwa upande wa uongo unapaswa kutambua mapema na kukiri au kujirekebisha.
Kuendelea kutetea uongo kunaendelea kuukuza zaidi kiasi cha kufikia hatua ambayo ni mbaya zaidi.
Wengi waliojikuta kwenye uongo mkubwa walianza na uongo mdogo kabisa.
Ni katika kuficha uongo huo ndiyo wakajikuta wakizidi kutengeneza uongo mkubwa.
Hatua ya kuchukua;
Epuka sana kujieleza na kujitetea kulikopitiliza.
Kama upo upande wa ukweli kufanya hivyo ni kuudhoofisha ukweli huo.
Na kama upo upande wa uongo kufanya hivyo ni kuukuza zaidi uongo huo.
Tafakari;
Watu hutilia mashaka maelezo na kujitetea kunakofanyika kwa nguvu kubwa.
Hakuna njia rahisi ya kunasa kwenye mtego wa wengine kama kupitia maelezo yako mwenyewe.
Utulivu unahitajika kwenye jambo lolote unalokuwa unapitia.
Kocha.