2634; Lakini unakosea.

Hayo ni maneno utakayoyasikia maisha yako yote, mpaka siku unayoondoka hapa duniani.

Kwa maamuzi yoyote utakayofanya na chochote utakachofanya, kuna watu watakuambia unakosea.

Sema unataka fedha na hicho ndiyo kipaumbele chako cha kwanza na kuna watu watakuambia unakosea, una tamaa sana ya fedha na fedha siyo kila kitu.

Sema hutaki fedha na wala siyo kipaumbele chako cha kwanza na kuna watu watakuambia unakosea, maisha yako ni magumu kwa sababu hujali kuhusu fedha na unapoteza fursa nzuri za kupata fedha zaidi.

Hakuna kitu chochote cha maana utakachoamua au kufanya kwenye maisha yako na wasijitokeze watu wakakuambia unakosea.

Hivyo usibadili maamuzi yako kutokana na maoni ya watu kwako kama unakosea au la.
Badala yake simamia maamuzi yako kutokana na umuhimu wake kwako.

Jua kwa hakika nini unataka kwenye maisha yako, jua ni kwa namna gani unapaswa kukipata kisha pambana mpaka ukipate bila ya kujali wengine wana maoni gani.
Muhimu tu ni kisiwe kinyume na sheria na kanuni za maadili.

Hakuna yeyote aliyefanya makubwa aliyekubaliwa na wale waliokuwa wanamzunguka.
Watu ni rahisi kuona makosa kuliko nia halisi ya mtu.

Mara nyingi watu wanapokuambia unakosea, hawakuongelei wewe, bali wanajiongelea wenyewe.
Wanamaanisha kwa mitazamo yao na nia zao, unachofanya siyo sahihi.
Hivyo ni wao, siyo wewe na hapo wako sahihi kabisa.

Usipoteze muda na nguvu zako kubishana na watu kwamba hukosei, wewe endelea kufanya, matokeo ya mwisho ndiyo yatakuwa hakimu mzuri.

Hatua za kuchukua;
Watu wanapokuambia unakosea, angalia wanamzungumzia nani, mara nyingi ni wao wenyewe.
Kama unalijua kusudi lako na tayari una ndoto kubwa.
Kama tayari una malengo na mipango ya kuishi kusudi lako na kufikia ndoto hizo.
Na kama hufanyi chochote kilicho kinyume na sheria za nchi, za asili na misingi ya maadili.
Basi hupaswi kumsikiliza yeyote anayekuambia unakosea.
Wapuuze na endelea na juhudi zako.

Tafakari;
Watu hupenda kuongelea mambo yao kupitia wengine.
Ambacho hawawezi wanawaaminisha wengine nao hawawezi.
Ambacho wanakosea wanawaaminisha wengine pia wanakosea.
Usikubali kubeba udhaifu huo wa wengine, simama kwenye mambo yako.

Kocha.