2638; Ni kujenga, siyo kuota.

Mafanikio huwa yanaanza na ndoto, mtu kuwa na picha ya kile unachotaka, ambacho kwa sasa huna.

Lakini ili kufikia ndoto hiyo, ni lazima ujenge.
Ndoto haitafikiwa tu kwa kuota,
Bali itafikiwa kwa kujenga.

Hatua unazochukua katika kuifikia ndoto ndizo zinaifanya ndoto hiyo kuwa uhalisia.

Thamani unayotoa kwa wale unaowalenga ndiyo inakuwezesha kufikia ndoto zako kubwa.

Hivyo ukishakuwa na ndoto kubwa, usiendelee kulala kitandani ukiziota au kupiga kelele kuwaambia wengine.

Badala yake kazana na kujenga yale yanayohitajika katika kufikia ndoto hizo.
Jenga biashara kama njia kuu ya kutoa thamani kwa wengine na wao kuwa tayari kukupa fedha.

Jenga uwekezaji kama njia kuu ya kutunza utajiri na kukufikisha kwenye uhuru wa kifedha.

Jenga ubobezi wako binafsi kama njia kuu ya kuacha alama hapa duniani.

Jenga mahusiano yako na wengine kwa sababu unawahitaji sana kwenye maisha yako.

Maisha ni ujenzi, kila wakati pambana kujenga.

Hatua za kuchukua;
Kila siku unayoianza, jiambie ni siku ya ujenzi. Kisha weka kwenye orodha vitu unavyokwenda kujenga kwa siku hiyo.
Kuongea na wateja wapya na kuwashawishi kununua ni sehemu ya ujenzi wa biashara.
Kila siku fanya kitu katika kujenga maisha yako ya mafanikio.

Tafakari;
Dunia ina wajenzi na wapiga debe. Wajenzi wanajenga vitu mbalimbali, wapiga debe ni mashabiki wa kila kitu.
Chagua unataka kuwa upande gani, ukijua wazi wanaofanikiwa ni wajenzi, huku mashabiki wakibaki vile walivyokuwa.

Kocha.