2641; Dawa kuu ya hasira.

Ni kupuuza.
Chukua mfano huu.
Wewe hujui lugha ya kireno.
Umekutana na mreno,
Halafu akakutukana kwa kireno.
Je utakasirika?

Jibu ni hapana,
Hutakasirika,
Kwa sababu hutajua hata kama amakutumana.

Kimbembe sasa ni unapokutana na mswahili mwenzako.
Akakuambia wewe ni mpumbavu kabisa.
Kinachotokea ni unaanza kujichaji mwenyewe.
Unaanza kujiambia; ameniita mpumbavu, amenichukuliaje, hajui mimi ni mtu na heshima zangu.
Unaendelea kujichaji zaidi; lazima nimfanyie kitu, la sivyo mazoea yataendelea.

Hapo ndipo hasira zinafika kileleni na unajibu au kufanya kitu ambacho baadaye unakuja kukijutia.

Dawa kuu ya hasira ni kupuuza.
Kila unapojikuta unaanza kujichaji, katisha haraka na puuza.
Chukulia kama hukusikia,
Au kama hilo huwezi chukulia mtu huyo ana matatizo yake binafsi.

Haijalishi mtu amesema au kufanya nini, usiruhusu hilo kuingia kwenye umakini wako na kuibua hasira.
Puuza kwa haraka sana jambo lolote linalokukwaza ili udumishe utulivu wako wa ndani.
Maana bila ya utulivu wa ndani, hii safari ya mafanikio itakuwa ngumu sana kwako.

Hatua ya kuchukua;
Usipatwe na hasira tena.
Puuza kila kitu kinachoanza kuibua hasira ndani yako.
Pale unaposhindwa kupuuza, kaa kimya na usiseme au kufanya chochote.
Na kubwa kabisa, kuwa ‘bize’ sana na malengo yako, yafanye yakuchoshe sana kiasi kwamba hupati muda wala nguvu za kuhangaika na mambo madogo madogo.

Tafakari;
Hasira hazitokani na kile ambacho mtu amesema au kufanya.
Bali zinatokana na tafsiri yako binafsi kwenye hayo.
Acha kutafsiri mambo kwa namna hasi na utatibu hasira.

Kocha.