2649; Jua likishachomoza umekwisha.

Kwa zama tunazoishi sasa, muda ni tatizo kwa kila mtu.
Mambo ya kufanya ni mengi na yanaongezeka kila siku.
Ila muda tulionao ni ule ule.

Kila mtu anawinda muda wetu kwa namna fulani.
Hivyo kikwazo kikubwa kabisa kwenye muda ni watu wengine.
Pale wanapohitaji tufanye mambo mbalimbali.

Mbaya zaidi inakuja pale ambapo mambo hayo ambayo wengine wanatutaka tuyafanye ni muhimu.
Kama umeajiriwa bosi wako anaweza kukupa majukumu fulani ambayo ni tofauti na mipango yako.

Kama umeajiri wafanyakazi wako wanaweza kuleta kwako matatizo na changamoto mbalimbali ambazo unapaswa kuzishughulikia.

Na hapo hujahesabu wale wanaokutafuta kwa njia mbalimbali za mawasiliano, wote wakitaka muda na umakini wako.

Yote hayo yanakufanya ugawe muda wako adimu kwa watu wengine na kujisahau wewe mwenyewe.
Kwa siku nzima unajikuta unawapa watu muda wako, ila wewe hupati muda kwa ajili yako mwenyewe.

Njia pekee ya kuvuka hili ni kwenda kinyume na watu walivyo, kujipa muda wakati ambapo hakuna anayetaka muda wako.

Na wakati mzuri wa kufanya hivyo ni asubuhi na mapema, kabla jua halijachomoza na dunia kuamka.

Wakati watu wamelala, uko huru kujipa muda wako bila ya kupata usumbufu kutoka kwa wengine.
Ni nadra sana mtu akakutafuta kwa siku alfajiri au kuanza kukupa majukumu muda huo.

Hivyo ushindi pekee kwako ni kulishinda jua, kuamka kabla jua halijachomoza na kupata muda kwa ajili yako.
Muda huo unautumia kusoma, kuandika na kuweka mikakati yako mingine.

Jua likishawaka tu, umekwisha, maana dunia inaamka na kuanza kuleta usumbufu wake kwako.
Watu wanaanza kukutafuta kwa mambo mbalimbali.

Pambana sana upate muda kwa ajili yako kabla ya jua kuchomoza.
Na katika muda huo, usiruhusu usumbufu wa aina yoyote ile.

Hatua ya kuchukua;
Hakikisha asubuhi na mapema kabisa unakuwa na muda kwa ajili yako. Isiwe chini ya saa moja na inaweza kuwa zaidi ya hapo kadiri uwezavyo.
Ukiamka saa 11, unapata angalau saa moja. Ukiamka saa kumi unapata masaa mawili.
Hakikisha unaweza kuamka asubuhi na mapema na kutenga muda huo kwa ajili ya maendeleo yako binafsi. Dunia ikishaamka inakuja na matakwa yake kwako hivyo huwezi kupata muda tena.

Tafakari;
Njia bora ya kupata muda kwa ajili yako ni wakati dunia imelala.
Ushindi muhimu kwenye siku yako ni kuamka kabla ya jua kuchomoza.
Kila siku pambana kupata ushindi huo ili uweze kujenga maisha ya mafanikio.

Kocha.