2650; Hujakitaka kweli.
Hadithi tulizokuwa tunaambiwa utotoni zilikuwa na mafunzo makubwa kuhusu maisha ambayo haikuwa rahisi kuyaelewa kwenye kipindi cha utoto.
Chukua mfano wa sungura aliyeziona ndizi na kuanza kuzirukia.
Mwanzo aliona ndizi ni nzuri na zinamfaa.
Kaanza kuzirukia lakini akawa hazifikii.
Karuka tena na tena ila hakuzifikia.
Mwisho akaamua kwamba hazitaki ndizi hizo, kwa sababu kwanza ni mbichi.
Pamoja na masomo mengi unayoweza kupata kwenye hadithi hiyo, kubwa ambalo wengi hawalipati ni umuhimu wa kukitaka kitu kweli, wa kutokuwa na mbadala mwingine.
Unapokitaka kitu kweli, unapokosa mbadala mwingine, unahakikisha kwa kila namna umekifanya.
Hutajipa sababu yoyote kwa nini huwezi kufanya.
Kwa kila namna utahakikisha unakifanya, maana hakuna mbadala.
Hivyo kama unakuwa na sababu yoyote inayokuzuia kufanya kitu, tatizo siyo hiyo sababu, bali tatizo ni wewe mwenyewe.
Unapokitaka kitu kweli hakuna sababu inayoweza kukuzuia.
Kama unakimbizwa na mbwa mkali na mbele yako kuna ukuta mrefu, unajikuta umeshapanda ukuta huo bila hata ya kujua umefanyaje.
Lakini katika hali ya kawaida hakuna namna unaweza kupanda huo ukuta, utakuwa na sababu za kila aina na zitaonekana ni sahihi, lakini ukweli ni hakuna uhitaji mkubwa wa wewe kufanya hivyo.
Kwa sababu zozote zile unazojipa kwa nini hujafanya au hujapata kitu fulani, jikamate na ujiambie ukweli kwamba hujakitaka kitu hicho kweli.
Angalia kama kweli umejitoa kwa kila namna na huna mbadala mwingine.
Maana ukishakuwa na mbadala, hakuna namna utaweza kufanya, sababu za kutokufanya zitakuwa nyingi kuliko za kuweza kufanya.
Hatua ya kuchukua;
Angalia mambo yote ambayo umekuwa unaahirisha kufanya au kushindwa kabisa kuyafanya. Jiulize swali la uhakika kwamba kwa nini huyataki kweli? Ni kwa namna gani maisha yako hayawezi kuathirika hata kwa kuyakosa hayo?
Kwa yale ambayo ni muhimu kabisa, yatake kweli, jiweke kwenye nafasi ambayo huna namna bali kufanya.
Na hapo sababu za kufanya zitakuwa kubwa kuliko za kutokufanya.
Tafakari;
Mtu anayezama kwenye maji hahitaji hamasa yoyote ili kujiokoa, kutetea uhai wake ni hamasa tosha.
Hivyo kama unashindwa kufanya kitu tatizo siyo kukosa hamasa, tatizo ni kutokukitaka kweli.
Unapokitaka kitu kweli na kutokuwa na mbadala mwingine, utafanya kila namna kukipata.
Kocha.