2652; Kuchuma matunda ya chini.

Ukiingia kwenye shamba jipya la matunda kama miembe au michungwa, inakuwa rahisi kuchuma matunda hayo.
Kwa sababu yanakuwa yananing’inia kwa chini na karibu kabisa kufikia kwa mkono.

Utaona hiyo ni fursa na kuifurahia, kwa kuwa unayapata matunda kirahisi kabisa, bila ya kutumia nguvu kubwa.
Lakini kadiri muda unavyokwenda, matunda ya chini yanaisha na hivyo inakubidi upande juu ili kupata matunda.

Hapo ndipo wengi huona fursa imeisha na kuamua kuachana na kitu hicho na kwenda kutafuta kingine.

Mfano huo wa matunda ya chini upo kwenye maeneo mengi ya maisha yetu.
Eneo moja kubwa ambalo mfano huu upo sasa ni kwenye biashara.

Unapoanza biashara, mwanzoni inakuwa rahisi kupata wateja. Kwa kuanza na watu wa karibu, watu wanaotaka kujaribu vitu vipya n.k.
Hilo litakufanya uone kuna fursa kubwa kwenye hiyo biashara.

Lakini baada ya muda unakuwa umewamaliza wateja hao rahisi kuwapata. Na hapo ndipo unapohitajika kuweka kazi ya ziada ili kupata wateja wapya zaidi.
Hili wengi huwa hawaliwezi na hivyo kuona fursa imeisha na kuachana na kitu hicho.

Mara zote jua kwenye kila kitu kipya unachoanza, kuna matunda ya chini ambayo ni rahisi kuyachuma.
Matunda hayo huwa hayadumu kwa muda mrefu, hivyo jiandae kuweka juhudi kubwa kupata matunda ya juu zaidi.

Hatua ya kuchukua;
Jitathmini kwa sasa ujue kama upo kwenye kuchuma matunda ya chini au ya juu. Mara zote jua kuna matunda ya juu zaidi, ambayo inahitajika kazi kuyafikia na wengi hawapo tayari kuweka kazi hiyo.
Hivyo kama wewe utakuwa tayari kuweka hiyo kazi, fursa zitaendelea kuwepo kila wakati.

Tafakari;
Kila urahisi huwa una mwisho wake, kwa sababu kila mtu anaukimbilia.
Mwisho wa urahisi siyo mwisho wa fursa, bali ni mwanzo wa fursa kubwa zaidi ambazo wengi hawaziwezi.

Kocha.