2655; Tatizo lako umekosa msimamo.

Unakumbuka ile siku ambayo ulihudhuria semina, ukajifunza mambo mengi na kutoka na hamasa ya kwenda kuyabadili kabisa maisha yako.
Siku chache za mwanzo ukawa wa tofauti kabisa, ukijituma kweli kweli. Lakini baada ya muda ukarudi kwenye mazoea yako.

Unakumbuka mara zote ambazo umekuwa unasoma vitabu na kujifunza mbinu mbalimbali za mafanikio. Ukazielewa kweli na kuona zinaweza kukusaifia, ukaanza kuzifanyia kazi na matokeo mazuri ukaanza kuyaona. Lakini baadaye ukarudi kwenye mazoea.

Unakumbuka mara zote umewahi kupata hadithi za watu waliofanikiwa, ukahamasika sana na kuanza kuishi kama wao, kuamka mapema, kujituma zaidi na mengine mengi.
Lakini haikuchukua muda ukawa umerudi kwenye mazoea.

Rafiki yangu, kila mmoja wetu anapitia hali za aina hii mara kwa mara.
Unajua kabisa nini unapaswa kufanya ili ufanikiwe.
Unaanza kabisa kufanya.
Lakini hufiki mbali, unaishia kuacha.

Kukosa msimamo ndiyo kikwazo kikubwa kwa walio wengi kufanikiwa.
Na wala huhitaji kuwaangalia wengine ndiyo ukubali hilo.
Anza tu kwa kujiangalia mwenyewe.
Jiulize kwa yote ambayo umewahi kujaribu kwenye maisha yako na kuacha, kama ungekuwa umechagua kimoja tu na kuweka juhudi zako zote bila kuacha ungekuwa wapi sasa?

Hata asili inatudhihirishia nguvu ya msimamo.
Tone moja la maji halina madhara yoyote kwenye mwamba.
Lakini matone yanayojirudia rudia kwa muda mrefu bila kuacha yana nguvu ya kuvunja mwamba mkubwa.

Hatua ya kuchukua;
Kwa matatizo yoyote unayopitia kwenye maisha yako, jiulize ni msimako gani umeukosa. Maana kila tatizo unalokutana nalo, chanzo chake ni kukosa msimamo.
Kuwa na msimamo kwenye kitu chochote kile na utaweza kufanya makubwa sana.

Tafakari;
Watu wanaweza kukuzidi akili, elimu, ‘koneksheni’ na vingine vingi. Lakini usikubali yeyote akuzidi msimamo kwenye kuweka kazi kwenye lile eneo ulilochagua. Wacha wengine wahangaike na mengi watakavyo, wewe weka msimamo kwenye kile ulichochagua.
Matokeo yanaweza yasionekane haraka, ila hilo halimaanishi kwamba hayapo, yanakuja, tena makubwa sana.

Kocha.