2656; Teknolojia itakunyoosha.

Siku siyo nyingi nilikuwa nataka kuwahi mahali na hivyo kuhitaji usafiri wa haraka wa pikipiki.

Nikitumia mtandao wa kuita vyombo vya usafiri na mara moja usafiri ukaja. Lakini dereva aliyekuja hakuwa mzuri, hakuendesha vizuri wala kufuata vyema maelekezo.

Pamoja na kumwambia lakini hakuonekana kusikiliza au kuelewa.

Basi nilipofika mwisho wa safari mtandao uliniuliza nitathmini safari, nikatoa nyota moja kati ya tano.
Mtandao ukauliza tatizo limekuwa nini, nikajibu tabia ya dereva haikuwa nzuri.
Mtandao ukanijibu utahakikisha dereva huyo hatokezi tena kwangu pale ninapoita usafiri.

Nimelitafakari hilo na kuona jinsi hii teknolojia inazidi kupata nguvu kubwa kwenye maisha yetu.
Zamani mtu uliweza kuwadanganya na kuwahadaa watu, kisha kwenda kwingine ambapo hujulikani na kwenda kurudia hilo.

Lakini kwa sasa teknolojia hairuhusu hilo, ukishafanya kitu, teknolojia inawajulisha watu wote kuhusu tabia yako.

Hivyo tunapaswa kuwa makini sana na kila tunachofanya, tukijua hakuna siri tena, teknolojia ina nguvu ya kuwafanya watu wajue tabia zetu halisi.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kila unachofanya, jua jicho la teknolojia linakumulika na kutunza kumbukumbu zako kwa miaka mingi ijayo.
Usijidanganye kuna siri tena kwenye zama hizi, kila unachofanya kipo wazi kwa dunia nzima.

Tafakari;
Teknolojia huwa haisahau, watu wengi wamekuja kupata vikwazo kutokana na mambo waliyofanya miaka mingi iliyopita, bila ya kujua madhara yake kwa baadaye.
Wewe kuwa makini na kila unachofanya ili usijitengenezee vikwazo vya baadaye.

Kocha.