2657; Huo mpango wako umekufikisha wapi?
Hatua ya kwanza kabisa katika kupata matokeo makubwa na ya tofauti ni kuwa na mpango tofauti.
Kufanya kile ambacho umekuwa unafanya, utaendelea kupata matokeo unayoyapata sasa.
Kile ambacho kimekufikisha hapo ulipo sasa, kitakubakisha hapo hapo.
Kama unataka kwenda zaidi ya hapo ulipo sasa, lazima kwanza ufanye kitu cha tofauti.
Usijidanganye, hakuna muujiza wa kupata matokeo tofauti kwa kufanya vile ulivyozoea.
Hivyo pale unapojiona umekwama, usiangalie sana matokeo unayoyapata, bali angalia hatua unazochukua, mchakato unaouweka.
Kila hatua unayofikia, jua ni kikwazo kwa hatua ya juu zaidi.
Kwa sababu utapenda kuendelea kufanya yale yaliyokufikisha kwenye hatua hiyo na yataendelea kukupa matokeo ya hatua hiyo.
Kwenda hatua ya juu zaidi, lazima ufanye vitu tofauti na ulivyozoea kufanya.
Hatua ya kuchukua;
Kila unapojiona unaweka juhudi kubwa lakini matokeo hayakuridhishi, tatizo siyo juhudi, tatizo ni mpango unaofanyia kazi.
Kama unafanyia kazi mpango ule ule, matokeo yatakuwa yale yale.
Tengeneza mpango tofauti ili kupata matokeo tofauti.
Tafakari;
Ukipanda maharage usitegemee kuvuna karanga. Haijalishi utakuwa na imani kiasi gani, haijalishi umeweka juhudi kubwa kiasi gani, maharage yataishia kuzalisha maharage.
Usianze kuhangaika na juhudi zako kabla hujahangaika na mpango wako.
Kocha.