2659; Tafuta changamoto zaidi.

Watu wengi hufikiri maisha yasingekuwa na changamoto ndiyo yangekuwa mazuri na yenye furaha.

Lakini ukweli ni kwamba maisha hayatakuja kukosa changamoto.
Kila wakati maisha yatakuwa na changamoto fulani.

Hata ukishakuwa na kila unachokitaka, ukawa na uhuru kamili wa kifedha, bado changamoto zitakuwepo tu.

Hata kama huhitaji kufanya kazi yoyote au kumridhisha yeyote, bado kuna changamoto zitaibuka kwako binafsi na hata kwa wengine pia.

Hivyo basi, badala ya kuzikimbia changamoto, unapaswa kuzitafuta zaidi.
Unapaswa kutafuta changamoto ambazo zinakupa fursa ya kukua zaidi ya pale ulipo sasa.
La sivyo utapata changamoto za kukudidimiza.

Na hii ndiyo maana unapaswa kuwa na ndoto kubwa sana unazozifanyia kazi kila wakati.
Ndoto ambazo kila mtu anaona haziwezekani.
Hizo zinakupa changamoto kubwa kiasi kwamba changamoto ndogo ndogo hazipati nafasi kwako.

Hebu fikiria unapambana kufikia ubilionea, kitu ambacho siyo rahisi hivyo kinakupa changamoto kubwa. Hivi unafikiri utajali sana wengine wanakuchukuliaje au nani kakusema vibaya?
Ukilinganisha na changamoto kubwa iliyo mbele yako, hayo mengine yanaonekana ni ujinga kabisa.

Unapojikuta unasumbuliwa na changamoto ndogo ndogo, dawa yake siyo kuziondoa, bali kutafuta changamoto kubwa zaidi kiasi kwamba hizo ndogo zinakosa nafasi kabisa.

Kwa kuwa maisha hayatakuja kukosa changamoto, jitengenezee changamoto zinazokusukuma ufanye makubwa zaidi kwenye maisha yako.

Hatua ya kuchukua;
Hakikisha unazo ndoto kubwa unazozipambania kila wakati, ndoto zinazofanya mengine yote yakose nguvu kabisa kwako.
Na ukishafikia ndoto hizo, weka nyingine kubwa zaidi.
Kila wakati hakikisha una changamoto kubwa unayofanyia kazi ili changamoto ndogo ndogo zisipate nafasi.

Tafakari;
Kusumbuliwa na changamoto ndogo ndogo ni kiashiria cha kutokuwa na changamoto kubwa na zenye manufaa.
Anza sasa kujiwekea changamoto kubwa ili ndogo ndogo zisipate nafasi ya kukusumbua.

Kocha.