#SheriaYaLeo (166/366); Kuwa mkali.

Mara nyingi huwa tunapenda kuwa wapole na wenye kujali wengine ili kuweza kuendana nao vizuri na kupata kile tunachotaka.

Hili huwa linafanya kazi vizuri wakati wa kawaida.
Lakini wakati wa hatari hilo linakuwa mzigo kwako, kufanya hivyo kunapelekea watu wakuone ni mtu unayefaa kuonewa, kukatishwa tamaa au kuzuiwa.

Mara kwa mara unapaswa kuwa mkali ili kuwafanya watu wajue wewe siyo mtu wa kuchukuliwa poa au kuonewa.
Lazima wajue kuna mambo ambayo huwezi kuyavumilia na yanapotokea uko tayari kupambana nayo kwa kila namna.

Hilo litawafanya watu wakuchukulie kwa hofu, kwa kuwa hawana uhakika utapokeaje jambo fulani wanaloleta au kufanya kwako.

Na kama Machiavelli alivyowahi kusema, ni bora kuhofiwa kuliko kupendwa, maana hofu unaweza kuidhibiti wakati upendo huwezi kuudhibiti.

Kutokuwa na uhakika ni bora kuliko vitisho; kama adui hana uhakika kukukabili kutamgharimu kiasi gani, hatakuwa tayari kujaribu hilo.

Sheria ya leo; Jijengee sifa ya ukali na kutokutabirika. Wafanye watu wajue inapokuja kwenye mambo yasiyo sahihi huwezi kuyavumilia. Pia wafanya wasiwe na uhakika juu ya hatua unazoweza kuchukua, hilo litapunguza sana mazoea yao kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji