2663; Ambacho hutumii nguvu kufanya.
Watu wamekuwa wanajiuliza sana ni njia ipi rahisi ya kufanikiwa.
Ni kipi ambacho wakifanya watafanikiwa.
Wamekuwa wakiwaangalia wale waliofanikiwa kwenye yale wanayoyafanya na kujaribu kuyaiga. Lakini bado hawafanikiwi.
Hawafanikiwi kwa sababu wanajaribu kuiga vitu vya nje,
Wakati mafanikio yanatokana na vitu vya ndani.
Mengi yameandikwa na kusemwa kuhusu mafanikio.
Lakini nikukumbushe na kukusisitizia kitu kimoja; mafanikio yako makubwa yapo kwenye kile ambacho hutumii nguvu kufanya.
Kile ambacho unakifanya bila kutumia nguvu au kutegemea msukumo mkubwa ndiyo chenye fursa kubwa ya mafanikio kwako.
Kwani hicho ndiyo utakachokifanya kwa muda mrefu bila ya kuchoka.
Nguvu za miili yetu zina ukomo na uhaba. Kama inabidi kujisukuma sana kufanya kitu, sehemu kubwa ya nguvu zako utaipotezea hapo na hivyo hutabaki na nguvu za kutosha kwenye ufanyaji.
Kama inabidi usukumwe sana ndiyo uweze kufanya kitu, hutapata wanaoweza kukusukuma kwa muda mrefu unaohitajika ili upate mafanikio makubwa.
Kama unaangalia sana matokeo kuliko unavyoangalia ufanyaji, pia safari ya mafanikio itakuwa ngumu kwako. Maana matokeo huwa hayaji haraka.
Ili usitumie nguvu kufanya kitu, ili usichoke na kuishia njiani, lazima upende sana kile unachofanya.
Lazima ukifanye kutoka ndani yako na siyo tu kuiga au tamaa.
Hatua ya kuchukua;
Kipi ambacho hutumii nguvu kubwa kufanya?
Kipi ambacho huchoki kufanya?
Kipi ambacho unapenda sana kufanya?
Mafanikio yako ndiyo yamejificha huko.
Fanya hicho zaidi na gatua vingine kwa wengine wakusaidie, utaweza kufanya makubwa sana.
Tafakari;
Watu huwa wanahangaika sana na siri za mafanikio.
Lakini ni jambo ambalo lipo bayana kabisa.
Fanya unachopenda au penda unachofanya na ukifanye kwa viwango vya juu kabisa.
Hilo litakutaka nguvu zako zote upeleke kwenye kile unachofanya na siyo uzipoteze kwenye kujisukuma kufanya.
Kocha.