#SheriaYaLeo (167/366); Tumia sanaa ya kuwepo na kutokuwepo.

Unapaswa kujua jinsi ya kupangilia kuwepo na kutokuwepo kwako.
Sisi binadamu huwa tunadharau kitu kinachopatikana muda wote na kuthamini kile ambacho hakipatikani.

Kwa ujumla, ni vyema kuegemea zaidi upande wa kutokuwepo/kutokupatikana ili pale unapokuja kuonekana watu wanakuwa na shauku kubwa.

Ukifanya hilo, kwenye kipindi ambacho haupo/haupatikani, watu watakuwa wanakufikiria na kukuongelea zaidi.
Hilo litaongeza sana thamani yako kwa wengine.

Kwenye zama hizi za mitandao ya kijamii, watu wamepoteza sana nguvu hii.
Watu wanapatikana sana, wanaweka kila kitu chao kwenye mitandao ya kijamii kiasi cha kila mtu kujua kila kinachoendelea kwenye maisha yao.

Hilo linaweza kuwafanya watu wakujue, lakini pia linawafanya wakuzoee na wakuone ni kama watu wengine wa kawaida.
Watu hawawezi kukuheshimu na kukuthamini kama unapatikana kirahisi na muda wote.

Tambua kwamba kuongea sana pia ni hali ya kuwepo/kupatikana na inafanya watu wakuzoee na kukupuuza.
Ukimya ni hali ya kutokuwepo/kutokupatikana ambayo inawafanya watu wakuthamini na kukuheshimu.
Pale unapozungumza, watu wanakusikiliza kwa umakini, maana hujazoeleka kuongea sana.

Katika hali hiyo pia pale unapokosea usijitetee wala kujieleza sana, badala yake kubali makosa na wajibika kwa kile kilichotokea.
Matendo yako yaonyeshe wazi kwamba umejifunza somo na umekuwa bora kuliko ulivyokuwa awali.

Sheria ya leo; Kama unapatikana muda wote na kwa urahisi, unaonekana wa kawaida na kudharaukika. Unapaswa kutengeneza hali ya kutokuwepo/kutokupatikana ili kuwapa watu nafasi ya kukufikiria na kukusubiria kwa shauku. Lakini pia ukipotea sana, watu wanakusahau kabisa. Hivyo mlinganyo sahihi kwenye kuwepo na kutokuwepo unahitajika ili kujenga mamlaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji