2670; UKIMWI, UKIRO na UKIA.
Unaujua UKIMWI, kifupisho na Upungufu Wa Kinga Mwilini.
Hii ni hali ambayo inaathiri mfumo wa kinga ya mwili, kiasi kwamba mwili unakuwa dhaifu na kushindwa kupambana na magonjwa.
Mtu mwenye UKIMWI ni rahisi kufa kwa ugonjwa ambao asiye na UKIMWI anaweza kupambana nao.
Hapa sitasema sana maana najua unajua UKIMWI ulivyo hatari n usivyokuwa na tiba mpaka sasa.
Lakini kwa ufupi, kitu chochote kinachoudhoofisha mwili, iwe ni kutokula vizuri, kutofanya mazoezi au kutokupumzika, kunauweka kwenye hatari ya kushambuliwa na maradhi mbalimbali.
Katika dhana hiyo hiyo, kuna maeneo mengine mawili huwa yanaathiriwa sana na kutuacha tukiwa dhaifu ila hatuna uelewa nayo.
Maeneo hayo ni ROHO na AKILI.
UKIRO ni Upungufu wa Kinga Rohoni. Hapa mtu anakuwa dhaifu sana kiroho kiasi kwamba changamoto ndogo ndogo za maisha zinamtikisa sana.
Roho ndipo ilipo nafsi yetu, hivyo ukiona mtu hajiamini, hajithamini na amekata tamaa kutokana na mambo mbalimbali anayopitia, jua ana UKIRO.
UKIRO ni hatari, japo wengi hawajui hili, ndiyo unapelekea watu kujiua, kudhuru wengine na hata kufanya mambo yanayowaweka kwenye changamoto kubwa zaidi.
Njia za kuondokana na UKIRO ni kujitambua wewe mwenyewe, kujua kusudi la maisha yako, kuwa na ndoto kubwa na kuamini kwenye kitu kikubwa kuliko wewe. Haijalishi imani yako kwenye dini au mambo mengine, lazima ujisalimishe kwenye nguvu ambayo ni kubwa kuliko wewe. Inaweza kuwa Mungu, Asili, Falsafa au kingine chochote. Muhimu ni ukiamini kweli na kukiishi kwenye maisha yako.
Na pale unapokutana na changamoto, huyumbishwi kwa sababu unajua imani yako ni kubwa zaidi ya chochote.
UKIA ni Upungufu wa Kinga Akilini. Hapa mtu anakuwa na udhaifu mkubwa wa kiakili kiasi kwamba anashindwa kung’amua mambo ya kawaida kabisa. Anashindwa kufikiri kwa kina na kufanya maamuzi sahihi. Anakuwa rahisi sana kudanganywa na kutapeliwa.
UKIA umekuwa hatari sana kwenye zama tunazoishi sasa, zama za maarifa na taarifa ambapo kuna mafuriko ya maarifa na taarifa. Kutokana na mafuriko hayo, ni vigumu mtu kuweza kufuatilia kwa kina kila kitu na kujua kipi ni sahihi na kipi siyo sahihi.
Taarifa zisizo sahihi zimekuwa zinasambaa kwa kasi sana na kupelekea watu kufanya maamuzi mabovu kwao.
UKIA ni hatari, kwani kuna wajanja wanautumia vizuri kupata kile wanachotaka.
Matapeli wote huwa wanatumia UKIA, wanaenda kwa mtu na fursa ambayo kwa wazi kabisa utaona haiko sawa. Lakini mtu akishakuwa na UKIA hawezi kufikiri kwa kina, hivyo anakubaliana nao na hapo ndipo anaishia kutapeliwa.
Chukua mfano huu wa kweli kabisa, mwenzetu amefuatwa na rafiki yake, akimweleza ufuta ni biashara inayolipa sana. Wakienda Mbeya na kuchukua eneo la kufanya biashara hiyo, kwa mtaji wa milioni 20 ndani ya miezi mitatu watakuwa wamepata milioni 40.
Kwa akili za kawaida, unaona wazi kabisa hicho ni kitu ambacho hakipo, maana kama kingekuwepo isingekuwa fursa tena, tayari wengine wangeshaifanyia kazi.
Lakini ukiwa na UKIA, unaona ni bonge la fursa, unaweka fedha, unazipoteza na kuishia kujihalalishia makosa uliyofanya.
Njia za kuondokana na UKIA ni kujifunza kwa kina, kutafakari mambo kwa kina na kudadisi na kuhoji kila kitu kabla ya kukubaliana nacho.
Lisha akili yako maarifa safi na sahihi ili kuweza kujenga uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.
Tafakari mambo kwa kina kabla ya kukimbilia kuamua. Angalia kila upande wa jambo, ona kila fursa na hatari iliyopo.
Na pia usiwe kama kondoo kufuata tu mkumbo, hoji na dadisi kila kitu. Jipe vigezo vya kufikia kabla hujakubaliana na kitu chochote.
Kwa zama hizi za mafuriko ya maarifa na taarifa unaweza kuona kama unachelewa kwa kufanya hayo. Lakini waswahili walishasema ni bora uchelewe na ufike kuliko kuharakisha na usifike.
Imarisha akili yako ili uweze kufanya maamuzi sahihi na yenye tija.
Hatua ya kuchukua;
Jitathmini kama una UKIMWI, UKIRO na UKIA.
Kwa UKIMWI siyo lazima uwe na virusi, huenda huli vizuri, hufanyi mazoezi au hupumziki kitu kinachodhoofisha mwili wako na kujikuta unashambuliwa na magonjwa mbalimbali.
Kwa UKIRO angalia jinsi unakabiliana na changamoto za maisha zinazokuja kwako, kama huridhishwi jiimarishe kiroho.
Na kwenye UKIA angalia maamuzi mbalimbali ambayo umekuwa unayofanya. Kama yamekuwa hayana tija basi jiimarishe kiakili.
Tafakari;
Miili yetu binadamu ina mfumo wa kinga kwenye kila eneo.
Unapoona kuna matatizo unayapata kwenye eneo fulani, jua tatizo linaanzia kwene kinga.
Kinga inapopungua ndipo matatizo na changamoto vinapata fursa ya kukusumbua.
Sisi binadamu ni ROHO, AKILI na MWILI. Eneo lolote hapo likikosa kinga, tunakuwa kwenye hatari kubwa.
Kocha.