2671; Wana ndoto, wasaidie wazifikie.
Falsafa kuu ya KISIMA CHA MAARIFA ni unawesa kupata chochote unachotaka kama utawasaidia wengi zaidi kupata kile wanachotaka.
Ndiyo, kuna vitu tunavitaka, ila kuvipata ni mpaka kwanza tuwasaidie wengine kupata vile wanavyotaka.
Kila mtu hapa duniani ana ndoto mbalimbali anazotaka kuzifikia.
Kwenye kila eneo la maisha yake kuna namna anataka kuwa.
Kuanzia kwenye afya, elimu, fedha, mahusiano n.k.
Wajibu wako mkuu, kwenye chochote unachofanya ni kujua ni ndoto gani ambazo watu wanazo.
Kisha jiulize unawezaje kuwasaidia wazifikie ndoto hizo kupitia kile unachofanya.
Kama unajihusisha na vitu vya ulaji na afya, jua ndoto ya wengi ni kuwa na afya bora. Je unawawezeshaje kufikia ndoto hiyo kupitia kile unachofanya?
Kama unajihusisha na mambo ya elimu, jua ndoto ya wengi ni kuwa na maarifa sahihi yanayowawezesha kufanya maamuzi bora. Je unawasaidiaje kufikia ndoto hiyo?
Kama unajihusisha na mambo ya fedha na mali, jua ndoto ya wengi ni kupata utajiri na kufikia uhuru wa kifedha. Je wewe unakuwa na mchango gani kwao kufikia hilo?
Japokuwa kuna kitu au vitu unavyotaka sana, hutavipata kwa kujiangalia wewe mwenyewe.
Bali utavipata kwa kuangalia unawanufaishaje wengine.
Hatua ya kuchukua;
Kwa kile unachofanya, waangalie wale unaowalenga kisha jiulize ni zipi ndoto zao kubwa.
Orodhesha ndoto zao hizo na jiulize unawasaidiaje ili waweze kuzifikia ndoto hizo.
Ukishajua jinsi ya kuwasaidia wengine kufikia ndoto zao kubwa, weka juhudi zako zote hapo, na kwa hakika utapata kile unachokitaka.
Tafakari;
Wajibu wako wa kwanza ni watu.
Kazi yako kubwa ni kuhakikisha wengine wameweza kufikia ndoto zao kubwa kupitia msaada wako.
Hapo ndipo watakuwa tayari kukupa kile unachotaka na wewe pia.
Hivyo usiangalie tu unapata nini kupitia watu, bali pia angalia watu wanapata nini kupitia wewe.
Kocha.