2676; Dawa ya njia za mkato.
Hebu fikiria wimbo mzuri sana ambao unapenda kuusikiliza,
Je utakuwa tayari kuuharakisha ili ufike mwisho?
Jibu ni hapana, uzuri wa wimbo siyo kuumaliza, bali kuusikiliza.
Kadhalika kwenye vitu vingine kama muvi, michezo na hata vitabu.
Kama kitu unakipenda, hutaki kiishe haraka.
Hata kwenye chakula na sherehe, kama ni nzuri hutaki iishe haraka.
Lakini inapokuja kwenye safari ya mafanikio, unataka iishe haraka, unataka njia ya mkato ya kukupa mafanikio makubwa bila kusumbuka.
Na unachoishia kupata kwenye njia hizo za mkato ni masumbuko makubwa zaidi.
Kwani njia hizo hazijawahi kufanya kazi, hata ziwe na ushawishi kiasi gani.
Dawa ya njia za mkato ni kufanya kile unachopenda kweli kutoka ndani ya moyo wako.
Kile ambacho mafanikio yako ya kwanza ni kukifanya.
Yaani kitendo cha kufanya tu, tayari ni mafanikio kwako, bila kujali matokeo gani unapata.
Unapokuwa unapenda kweli kile unachofanya, hupati muda wa kupoteza kuhangaika na njia za mkato.
Maana hizo zinakuondoa kwenye kile unachotaka kufanya kweli.
Hatua ya kuchukua;
Je umekuwa unahangaika na njia za mkato pamoja na fursa nyingi mpya zinazokuja kwako?
Tatizo ni hufanyi unachopenda au hupendi unachofanya.
Amua sasa kukipenda kweli kile unachofanya sasa.
Na kama hilo haliwezekani kiache na nenda kafanye kile unachopenda kweli kufanya.
Mafanikio ya kwanza kwako yanapaswa kuwa ni kufanya, matokeo ni kitu cha ziada.
Tafakari;
Kikwazo kikubwa cha mafanikio kwa wengi ni mapenzi.
Kama hupendi kweli kweli kile unachofanya, nafasi ya kufanikiwa ni sifuri.
Ndiyo kinaweza kukupa fedha, ambazo ni muhimu sana, lakini bado ndani yako kunakuwa na utupu mkubwa.
Hakikisha kile unachofanya unakipenda kweli, na hapo utakuwa na uhakika wa mafanikio.
Kocha.