2679; Kwamba wewe ni wa pekee sana?

Tunapojifunza hadhithi za wengine ambao wamepiga hatua, huwa tunafurahia sana hilo.
Tunaona wametoka chini na kupambana mpaka kufika juu.

Kwa kuangalia nyuma, tunaona wazi kwamba kufanikiwa kwao ilikuwa lazima, hakuna namna wangeweza kushindwa.

Lakini sasa inapokuja kwetu, tunaishia kutafuta sababu kwa nini hicho kilichowezekana kwa wengine hakiwezekani kwetu.

Na kwa kuwa tunatafuta sababu ya aina hiyo, huwa hatuikosi.
Lazima tutaipata tu.
Hata kama siyo sababu ya kweli, tutachukua yoyote na kwenda nayo.
Maana tunachotaka siyo ukweli bali kuridhika.

Kwa kuwa hatupo tayari kupambana kama wengine walivyopambana, tunaishia kujiridhisha kwamba kilichowezekana kwao kwetu hakiwezekani.

Ninachotaka ujiolize leo, je wewe ni wa pekee sana kiasi kwamba kile kinachowezekana kwa wengine kwako hakiwezekani au ni uzembe tu?

Unapoona wengine wamepiga hatua, usiangalie nini mnatofautiana, bali angalia nini mnafanana.
Maana vya kutofautiana huwa havikosekani, lakini vya kufanana vipo.

Na kama wao wanaweza, basi hata wewe unaweza.
Kinachohitajika ni kuamua, kujitoa na kutokukata tamaa.

Hakuna kitu bora ambacho ni rahisi, hivyo usichanganye kutaka kwako urahisi na kuona vitu haviwezekani.

Hatua ya kuchukua;
Acha kujidanganya kwamba wewe huwezi kupiga hatua kubwa kama ambazo wamepiga wengine.
Ukweli ni unaweza kupiga hatua kubwa kuliko hata wao.
Hivyo kila unapojiambia wewe ni tofauti, jikumbushe kwenye kufanya makubwa, tofauti pekee unayoweza kuwa nayo ni uvivu na uzembe.
Jitoe kweli kwa chochote kile na utaweza kufanya makubwa sana.

Tafakari;
Kama wengine wanaweza kufanya kitu fulani, hata wewe unaweza kukifanya, tena kwa viwango vya juu zaidi.
Hilo ndiyo unalopaswa kuliamini na kulifanyia kazi wakati wote.

Kocha.