Habari mwanamafanikio?
Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo kuna mambo mawili makubwa.
Jambo la kwanza ni mjadala wa kitabu cha GETTING TO YES, kitabu kinachotufundisha msingi sahihi wa kufanya majadiliano yenye manufaa kwa pande zote. Majadiliano hayo ya msingi yana hatua nne ambazo ni kuwatenganisha watu na tatizo, kuangalia maslahi ya pande zote, kutengeneza machaguo zaidi na kutumia vigezo vya msingi katika kufanya maamuzi. Kwenye kipindi tumejadiliana kuhusu haya ambapo wanamafanikio mbalimbali wameshirikisha yale waliyojifunza pamoja na uzoefu wao.
Jambo la pili ni mahojiano na mwanamafanikio mwenzetu Mtabazi Sahini ambaye anatushirikisha safari yake ya mafanikio kwenye eneo la taaluma na nje ya taaluma. Kitaaluma Mtabazi anatushirikisha safari yake ya elimu tangu shahada ya kwanza mpaka kupata PhD. Pia anatushirikisha jinsi aliweka lengo la kupanda cheo kutoka kuwa mhadhiri (Lecturer) mpaka kuwa mhadhiri mwandamizi (Senior Lecturer) kupitia kufanya tafiti na machapisho. Aliweza kupambania lengo hilo na ndani ya mwaka mmoja akaweza kulikamilisha.
Pia Mtabazi ametushirikisha mambo mengine ambayo amekuwa akifanya nje ya taaluma. Ametushirikisha kilimo cha pilipili alichowahi kufanya, uzalishaji wa vifaranga wa samaki, kituo cha mafunzo ya sayansi kwa vitendo na biashara ya samaki anayofanya kwa sasa. Mtabazi ameweza kupitia mengi katika safari yake ambayo yana somo kubwa kwake na kwa kila mmoja.
Karibu usikilize kipindi hiki uweze kujifunza na kwenda kuchukua hatua ili kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.
Kocha.