2680; Kilicho ndani ya uwezo wako kamili.

Kwenye safari ya mafanikio, huwa kuna kukwamishwa kwa aina mbalimbali.
Hasa pale tunapofanya vitu ambavyo vinawategemea wengine, ni rahisi kukwamishwa na hao tunaowategemea.

Lakini hupaswi kutumia hilo kama sababu ya kutokufanikiwa.
Hupaswi kusema wengine ndiyo waliokukwamisha.

Kwani haijalishi ni kipi unategemea mwenyewe, bado kuna sehemu kubwa ya mafanikio yako inakutegemea wewe mwenyewe.

Kwa chochote unachofanya, kuna upande ambao upo ndani ya uwezo na udhibiti wako kamili.
Na upande huo huwa una nguvu kubwa inayoweza kushinda changamoto ya kukwamishwa na wengine.

Upande ninaozungumzia hapa ni wa mchakato.
Kile unachopaswa kufanya wewe katika safari yako ya mafanikio.

Kwa mfano kwenye biashara, huwezi kudhibiti ni wateja wangapi watanunua na kwa muda gani.
Lakini unaweza kudhibiti ni wateja wangapi umeongea nao na kuwashawishi kununua.
Hivyo badala ya kuangalia matokeo ya wateja unaowapata kama kikwazo, wewe angalia idadi ya wateja wapya unaoongea nao kama mchakato.
Kama utaongea na wateja wapya 10 kila siku bila kuacha, ni lazima utapata wateja wengi, japo hujui lini na kwa kiwango gani.

Kadhalika kwenye uandishi, unaweza usijue ni vitabu vingapi utachapa na kwa wakati gani.
Lakini kama utajiweka kwenye mchakato wa kuandika kila siku bila kuacha, ni dhahiri utaweza kuchapa vitabu vingi.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye kila eneo la maisha, huna udhibiti wowote kwenye matokeo, ila una udhibiti mkubwa kwenye mchakato.
Sasa wajibu wako ni kukamilisha mchakato wako kwa asilimia 100 na kwa msimamo wa hali ya juu sana.
Halafu kuyaacha matokeo yaje kwa wakati wako.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kile kikuu ulichochagua kama njia ya kufikia mafanikio, ni sehemu ipi ipo ndani ya uwezo wako kamili?
Ni kipi ambacho unaweza kufanya kila siku bila ya kukwamishwa na yeyote?
Hapo ndipo unapaswa kuweka nguvu na umakini wako wote na kupuuza maeneo mengine yasiyo na tija.
Kama kweli unayataka mafanikio, hili ni la kuzingatia sana.

Tafakari;
Kabla hujalalamika wengine wanakukwamisha, hebu angalia ni kwa jinsi gani umekuwa unajikwamisha wewe mwenyewe.
Kutokuweka kwako jugudi kwenye mchakato na kukosa kwako msimamo kuna madhara makubwa kwako kuliko madhara yanayoletwa na ukwamishaji wa wengine.
Acha kujikwamisha wewe mwenyewe, weka juhudi kubwa kwenye mchakato na hakuna kitakachoweza kukukwamisha.

Kocha.