#SheriaYaLeo (188/366); Tumia mauzo laini.

Kama lengo lako ni kujiuza wewe mwenyewe, iwe ni kujenga ushawishi au unagombea nafasi fulani, kuna njia mbili za kufanya hivyo.

Njia ya kwanza ni kuuza kwa ugumu (hard sell). Hapa unaeleza moja kwa moja kila unachotaka, unaelezea mafanikio yako, unatumia takwimu mbalimbali na maoni ya wataalamu.
Unaweza kwenda mbali zaidi kwa kutumia hofu, kuwaonya watu hatari watakayokutana nayo kama hawatakubaliana na wewe.

Pamoja na njia hii kueleza ukweli ulivyo, baadhi ya watu hawatakubaliana na wewe. Watakasirishwa na namna unavyotaka kile unachotaka. Na watachukua kabisa hatua ya kukupinga na kukuwekea vikwazo.
Wengine wataona kama unawahadaa ili ujinufaishe wenyewe.
Wapo watakaokuwa na wasiwasi kwa nini unatumia nguvu nyingi sana kutaka unachotaka? Wataona kama una nia iliyojificha.

Njia ya pili ni kuuza kwa ulaini (soft sell). Hapa huelezi moja kwa moja kile unachotaka, bali unatumia vitu vingine ambavyo watu wanapenda, kisha unapenyeza lengo lako nyuma ya vitu hivyo.
Njia hii ina nguvu ya kuvutia mamilioni ya watu kwa sababu inawaburudisha na kuwaambia kile wanachotaka kusikia.

Kwa kutumia njia hii hakuna wanaokuchukia wala kukushambulia au kukukwamisha.
Kwa sababu huonekani kama kuna kitu unataka. Bali unaonekana kuwapa watu burudani na habari njema.

Njia hii imekuwa ikitumiwa tangu enzi na enzi na wauzaji, wanasiasa na hata matapeli.
Kwanza wanaandaa onyesho au tamasha la burudani ambapo watu wengi wanavutiwa kuhudhuria.
Wanawapa burudani ya kweli na hilo linawafurahisha sana.
Wakiwa katika hali hiyo ya furaha ndiyo wanapenyeza lengo lao.
Katika hali hiyo, wanakubalika kwa urahisi na bila ya kutumia nguvu kubwa au kutengeneza upinzani.

Kwa kuwa watu huwa hawabadiliki, njia hii bado inatumika na ina nguvu mpaka leo.
Angalia wanasiasa wanavyotumia wasanii.
Angalia wanaouza vitu kwa promosheni wanavyotumia wacheza muziki.
Na wewe tafuta onyesho au burudani itakayokusaidia kujiuza kwa namna unayotaka.

Sheria ya leo; Kamwe usionekane kama kuna kitu unauza moja kwa moja na kwa nguvu kubwa. Hilo litawafanya watu wakushuku na kukupinga. Badala yake wape watu burudani kwanza, wafanye wajisikie vizuri na kufurahia na hapo ndipo unapoweza kupenyeza mauzo yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji