2697; Usiwe na hatia.
Kila mtu anapenda kufanikiwa,
Lakini wengi hawajajipanga na madhara ambayo yanakuja na mafanikio.
Kama ambavyo dawa zinatibu ila zina madhara yake,
Ndivyo pia mafanikio yalivyo, ni mazuri ila huwa yanakuja na madhara yake.
Na madhara makubwa ya mafanikio ni kujengewa hali ya hatia.
Kwa kuwa mafanikio ni magumu, siyo wote wanaoweza kuyapata.
Hivyo ukipambana ukafanikiwa, wengi waliokuzunguka watakuwa hawajafanikiwa.
Ni hao ndiyo watakaokufanya ujione una hatia ili waendelee kukudhibiti licha ya mafanikio yako.
Kwa kuwa umeshafanikiwa kuliko wao, wanakuwa hawana njia nyinyine ya kukudhibiti isipokuwa hatia.
Hivyo basi, watakutengenezea kila hali za kukufanya ujione una hatia.
Watayageuza mafanikio yako kuwa kikwazo na maumivu kwao.
Watakufanya ujione ni mbaya na usiyejali wengine kwa sababu unapambana kujenga au kulinda mafanikio yako.
Watataka uwape vitu ambavyo hata wewe mwenyewe hujawahi kujipa na utakapokataa watasema una roho mbaya na hujali, yote hiyo kukufanya ujione una hatia.
Watakushauri vitu vya kufanya ambavyo havina tija na utakapokataa kuvifanya halafu ukakutana na changamoto, watakufanya uone ni kwa sababu hukufuata ushauri wao.
Na kubwa zaidi, pale watakaposhindwa wao, watatafuta kila namna ya kuleta lawama kwako.
Kwa mfano kama mtu ana mkopo benki ambapo ameweka nyumba yake dhamana, akashindwa kulipa mkopo huo na benki ikaja kuuza nyumba kwa mnada. Wewe ukinunua nyumba hiyo watakufanya ujione una hatia. Wataacha kuangalia uzembe wao wa kushindwa kulipa deni na kukulaumu wewe kwa kununua nyumba yao kwa mnada.
Au kama mtu biashara imemshinda na ukachukua eneo lake la biashara ili kukuza zaidi bishara yako, watafanya kila namna ujione una hatia. Hawataangalia jinsi wameshindwa biashara, bali wataangalia kwamba wewe umewaondoa kwenye biashara.
Tufanye nini?
Lazima tujue wazi kwamba kadiri tunavyofanikiwa ndivyo tunavyowaacha nyuma wale waliotuzunguka.
Hilo halitawafurahisha na hivyo watatutengenezea hali ya kuwa na hatia.
Hatupaswi kujiruhusu kuwa na hatia kwa namna yoyote ile.
Tunachopaswa kufanya ni kile kilocho sahihi mara zote.
Watu wanakichukuliaje siyo wajibu wetu, ni matatizo yao wenyewe.
Lazima tujue wengi hawatafurahia mafanikio yetu na hilo lisitupe tabu hata kidogo.
Badala yake tuendelee na juhudi za kupata mafanikio zaidi.
Hatua ya kuchukua;
Usikubali kuwa na hatia (have no guilt) kwenye jambo lolote lile. Fanya kilicho sahihi mara zote na songa mbele, watu wanatafsirije au kutengeneza vitu gani siyo biashara yako.
Na pale unapokosea, kubali na miliki kosa lako kisha songa mbele. Usikubali kubaki kwenye hatia, ni njia ya walioshindwa kukuzuia usifanikiwe zaidi.
Tafakari;
Watu ambao hawajafanikiwa huwa wana uwezo wa kutengeneza mazingira ya kuonyesha wale waliofanikiwa ndiyo chanzo cha wao kutokufanikiwa.
Jua hili mapema na lizingatie unavyopambana na mafanikio yako.
Usikubali kuwa na hatia kwenye jambo lolote lile.
Kuwa huru, kuwa safi na umakini wako wote peleka kujenga mafanikio zaidi na siyo kutaka kumridhisha kila mtu.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining