2708; Usiombe ruhusa, usiombe samahani.

Kitu kikubwa kuhusu maisha ya mafanikio ni huwezi kuw kama watu wengine.
Huwezi kuishi maisha ambayo wengine wanayaishi na kutegemea upate mafanikio makubwa kabisa.

Ni lazima maisha yako yawe ya tofauti kabisa na maisha ya wengine.
Na njia moja ya kuonyesha tofauti hiyo ni kutokuomba ruhusa au samahani.

Hii ni dhana muhimu sana ambayo ukiweza kuielewa na kuiishi, maisha yako yatakuwa rahisi sana na utaweza kufanya makubwa.

Kutokuomba ruhusa au samahani haimaanishi kuwa mkorofi na usiyeambilika.
Badala yake inamaanisha kuishi maisha ambayo huhitaji kuomba ruhusa wala samahani.

Kutokuomba ruhusa maana yake unapaswa kuwa na maisha huru ambayo unaweza kufanya chochote unachotaka kufanya bila ya kuomba ruhusa ya mtu yeyote yule.
Hiki ni kiwango cha juu kabisa cha uhuru kwenye maisha.
Unapofikia kiwango hiki unakuwa na uwezo wa kufanya makubwa sana.
Hakuna yeyote anayeweza kukuzuia kufanya yale muhimu yanayokupa mafanikio yako.

Kutokuomba samahani maana yake unapaswa kuishi maisha ambayo hakuna kitu unachofanya kinachokulazimu uombe samahani kwa wengine.
Maana yake unakuwa umejiwekea misingi yako mwenyewe kwenye maisha na kuiishi misingi hiyo bila ya kuivunja.
Hilo linakufanya mara zote ufanye kile kilicho sahihi bila kukosa.
Na kwa kufanya hivyo, huhitaji kumwomba yeyote samahani.
Maana unaishi kwa misingi sahihi uliyojiwekea, kama mtu anakasirishwa na misingi yako, hakuna namna unaweza kumsaidia.

Kutokuomba ruhusa wala samahani haimaanishi kuishi maisha ya kihuni na kutokujali.
Bali inamaanisha kuishi maisha rahisi na yanayofuata misingi sahihi.

Hatua ya kuchukua;
Jijengee uhuru kwenye maisha ambapo hulazimiki kumwomba mtu yeyote ruhusa ndiyo uweze kufanya kile unachotaka kufanya.
Pia kuwa na misingi unayoiishi wakati wote ili usihitajike kuomba samahani kwa wengine.

Tafakari ya leo;
Kama kila wakati inabidi uombe ruhusa kwa wengine ndiyo uweze kufanya unachotaka, hao unaowaomba ruhusa ndiyo kikwazo kwa mafanikio yako.
Kama kila wakati unalazimika kuwaomba wengine samahani, huna misingi unayoiishi na hilo litakukwamisha sana.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining